tmoja2

Agizo la Waziri Mkuu kwa viongozi wanaowasimamisha na kuwafukuza kazi Watumishi wa umma

308
0
Share:
Share this
tmoja2

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Kassim amewataka viongozi wote katika wizara, taasisi, na idara mbalimbali za kuzingatia utawala wa sheria na kanuni za utawala bora na kuacha mara moja utaratibu wa kusimamisha au kuwafukuza kazi watumishi waliopo chini yao bila kufuata matakwa ya sheria.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo jana wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Sita wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) katika ukumbi wa Mwalimu Julius K. Nyerere uliopo Chuo cha Mipango, nje kidogo ya mji wa Dodoma.

Akijibu hoja iliyokuwa imetolewa kuhusu wafanyakazi kuwekwa ndani kiholela, kunyanyaswa, kushushwa vyeo na kusimamishwa kazi na wanasiasa, Waziri Mkuu alisema kuwa, Serikali chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Magufuli itaendelea kuzingatia utawala wa sheria na kanuni za utawala bora ili kuhakikisha kuwa haki za wafanyakazi zinalindwa ipasavyo.

“Kimsingi watumishi wanasimamiwa na mamlaka za kinidhamu na sheria mbalimbali ambazo hazina budi kuangaliwa kwa pamoja kabla ya kuchukua hatua. Ninawaagiza viongozi wenzangu wa kisiasa na walioko katika wizara na taasisi zote za Serikali, mikoani, wilayani, kwenye idara za Serikali na Halmashauri wazingatie utawala wa sheria wakati wa kushughulikia masuala mbalimbali yanayohusu wajibu na haki za wafanyakazi,” alisema Waziri Mkuu

Wafanyakazi wengi wamekuwa wakilalamikia vitendo vya viongozi mbalimbali kuwasimamisha kazi, kuagiza wakamatwe na hata kuwafukuza kazi bila kufuata kanuni na sheria. Sheria inataka kuwa mfanyakazi au mtu yeyote anapotuhumiwa kwa kosa lolote lile, lazima apewe nafasi ya kusikilizwa.

Kauli hii ya Waziri Mkuu imekuja saa chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuagiza kukamatwa kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Gogo la Mboto, Bakari Shingo baada ya mkazi wa eneo hilo kumtuhumu kuwa ametengeneza risiti bandia.

Comments

error: Content is protected !!