Askofu akutwa na hatia ya ufisadi mali za kanisa, avuliwa Uaskofu

559
0
Share:
Share this
CMTL Group

Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dokta Valentino Mokiwa amakataa kuachia wadhifa huo baada ya  Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dokta Jacob Erasto Chimeledya kutangaza kuwa wamemvua Dkt Mokiwa wadhifa wake kufuatia makosa ya utovu wa nidhamu aliyoyatenda.

Askofu Mokiwa aliupinga uamuzi huo na kuongeza kuwa Askofu Chimeledya hana mamlaka ya kumvua madaraka sababu yeye si muajiri wake na kuwa anayeweza kumvua madaraka ambaye ni muajiri wake ni Sinodi ya Dar es Salaam.

Uamuzi wa kumvua cheo hicho ulikuja baada ya Askofu Mokiwa kutiwa hatiani kwa kufuja mali za kanisa kinyume na maadili ya kiuchungaji ambayo yaliainishwa katika ripoti ya uchunguzi. Maaskofu kadhaa walimshauri Askofu Mokiwa kuwa ajiuzulu lakini yeye alikataa.

Mashtaka 10 yakiwemo ya ufisadi wa mali za kanisa yalifunguliwa na walei 32 wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam ambayo pia yalichangia Askofu Mkuu wa Anglikana Tanzania kufikia uamuzi wa kumvua Uaskofu Dkt. Mokiwa.

Askofu Chimeledya baada ya kutangaza kumvua uaskofu Dkt Mokiwa, aliagiza waraka wa kanisa hilo unaoonyesha kuvuliwa Uaskofu usambazwe katika makanisa ya Anglikana Tanzania ili usomwe katika ibada za Januari 8.

Kwa upande mwingine, viongozi wengine wa Dayosisi ya Dar es Salaam wanasema sio kweli kwamba Askofu Mokiwa amevuliwa cheo hicho sababu uamuzi wa Askofu Chimeledya haukufuata taratibu, hauna baraka za Sinodi ya Dar es Salaam na hata barua zilizosomwa jana makanisani zilizomwa kimakosa.

Comments

error: Content is protected !!