Fahamu sababu za kwanini vigogo wa Escrow huenda wasifikishwe katika Mahakama ya Mafisadi

436
0
Share:
Share this
CMTL Group

Ikiwa ni takriban miezi sita tangu kuanzishwa kwa Divisheni Maalum ya Mahakama ya Rushwa na Ufisadi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Vigogo waliotuhumiwa kwa kashfa kubwa zilizotikisa nchi miaka ya nyuma likiwamo sakata la uchotwaji wa fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, hawatashtakiwa katika mahakama hiyo, imefahamika.

Divisheni hiyo maarufu kwa jina la Mahakama ya Mafisadi, ilianza kazi rasmi Julai 8, mwaka jana ikiwa ni moja ya ahadi zilizonadiwa na Rais John Magufuli katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-­2020 wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi.

Wakati kukiwa na matarajio kwamba Mahakama ya Mafisadi itashughulika na vigogo wanaodaiwa kushiriki katika kuihujumu nchi kupitia kashfa mbalimbali za kifisadi ikiwamo hiyo ya akaunti ya Tegeta Escrow, divisheni hiyo nyeti ya Mahakama Kuu haitakuwa na meno dhidi yao.

Hata vigogo wanaodaiwa kutafuna mabilioni ya fedha za kupitia sakata la Kampuni ya Lugumi Enterprises na Jeshi la Polisi nao hawatafikishwa mbele ya Mahakama hiyo ikiwa watabainika kuhusika katika kashfa hiyo.

UTAWALA WA SHERIA.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt Harrison Mwakyembe katika mahojiano maalum na chanzo cha habari hii, alisema kisheria isingekuwa sahihi kuyachukua makosa yaliyotendwa zamani na kuyapeleka mbele ya Mahakama ya Mafisadi.

‘Sisi ni Taifa linaloheshimu Utawala wa Sheria, ambao unazuia utoaji wa adhabu kwa makosa ya zamani kwa kutumia sheria mpya au vifungu vya sheria vipya. Kwa kiingereza tunaita sheria (au vifungu vyake) yenye ‘retrospective effect’. Hata Katiba ya nchi inazuia hili kutokea chini ya ibara ya 13(6)(c)’ alisema.

Ibara ya 13(6)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasema ” Ni marufuku kwa mtu kuadhibiwa kwa sababu ya kitendo chcochote ambacho alipokitenda hakikuwa ni kosa chini ya sheria, na pia kwamba ni marufuku kwa adhabu kutolewa ambayo kubwa kuliko iliyokuwapo wakati kosa linalohusika lilipotendwa”

Dk. Mwakyembe aliendelea kufafanua, Sheria ya uhujumu uchumi imefanyiwa marekebisho sio tu kwa kupanua wigo wa ma makosa kusikilizwa na Mahakama ya Mafisadi kama vile utakatishaji wa fedha haramu, ugaidi, makosa ya ukiukaji sheria za uhifadhi wa maliasili- wanyama, misitu na hata na hata kuyaongezea adhabu baadhi ya makosa.

-Nipashe

Comments

error: Content is protected !!