tmoja2

Historia ya meli kongwe Tanzania yenye zaidi ya miaka 100 ambayo bado inafanyakazi

250
0
Share:
Share this
tmoja2

Kwa miaka 101 sasa meli ya Kijerumani Graf von Götzen (sasa MV Liemba) imekuwa ikisafiri katika Ziwa Tanganyika ikisafirisha sio watu na mizigo yao, bali pia ikibeba utamaduni na historia pamoja nayo.

img-20161210-wa0037

Kigoma ni mkoa wa Magharibi ya Tanzania ulio kwenye ufukwe wa upande wa Mashariki wa Ziwa Tanganyika. Meli ya MV Liemba, inayomilikiwa na Shirika la Reli la Tanzania, hung’oa nanga katika mji huo, tayari kwa safari ya kuelekea Mpulungu, Zambia, na baadaye Kassanga, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiwa imebeba abiria na mizigo yao.

Hakuna anayeweza kusema hasa, ni safari ya ngapi meli hii ya Liemba imeng’oa nanga na kutweka katika bandari hii ya Kigoma. Lakini inafahamika kuwa, hii ni miongoni mwa meli chache duniani kuishi na kuendelea kufanya kazi kwa zaidi ya karne moja sasa. Hadi mwaka 2016, MV Liemba imetimiza miaka 101 kamili tangu ianze kuelea kwenye Ziwa Tanganyika, ikiwa imeletwa hapo na Wajerumani mwaka 1915.

img-20161210-wa0036

Historia ya Liemba

Meli ya Liemba ina historia ya kufurahisha. Mwanzoni iliitwa Graf von Götzen, ikipewa jina la gavana wa Kijerumani nchini Tanganyika. Iliamriwa kuletwa kwenye Ziwa Tanganyika na Mfalme Wilhelm wa Pili hapo mwaka 1913.

Ilipewa jina la Liemba, ambalo ni jina la asili ya upande wa Kusini wa Ziwa Tanganyika, na Waingereza katika miaka ya 1920 baada ya kuwashinda Wajerumani kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia, na kuizamua baada ya kuzamishwa kwa makusudi na majeshi ya Ujerumani.

img-20161210-wa0030

Meli hii iliundwa kwenye kiwanda cha meli cha Meyer-Werft Shipyard, mjini Papenburg, na kisha ikaunduliwa vipande vipande na kusafirikwa kwenye masanduku kutoka bandari ya Hamburg hadi jijini Dar es Salaam, ambao leo ni mji mkubwa wa kibiashara wa Tanzania.

Kutoka Dar es Salaam, masanduku hayo yalibebwa kwa treni hadi karibu na Kigoma, ambako kwa kuwa reli iliishia hapo, yakabebwa kwenye mabega ya watu hadi kwenye Ziwa Tanganyika. Haijulikani ni watu wangapi walifariki njiani wakiwa na shehena na vipande vya MV Liemba mabegani mwao!

Umuhimu wa MV Liemba

Hivi leo, Liemba inafanya safari zake baina bandari ya Kigoma kwa upande wa Tanzania na Mpulungu kwa upande wa Zambia, ikishusha na kupakia abiria na mizigo yao katika vituo kadhaa hapo katikati yake.

Na kama Joseph Bhwana anavyosema, Liemba imekuwa “meli pekee inayowaunganisha watu wanaolizunguka Ziwa Tanganyika na kwa kuwa kwake njia pekee ya usafiri wa uhakika kwenye ziwa hili, mtu anaweza kuuona umuhimu wa meli hii kwa mafungamano ya kijamii, kiuchumi na kitamaduni ya watu hawa.”

img-20161210-wa0031

Joseph Mbwiliza, aliyewahi kufanya kazi kama mtaalamu kwenye Wakfu wa Mwalimu Nyerere, anasema kwamba Liemba inakwenda mbali zaidi ya kuwa meli ya kusafirisha mizigo na watu tu, bali inatekeleza dhana ya soko la pamoja kwa nchi hizi.

“Tunatarajia sana kwamba Liemba itakuwa kiungo kikubwa cha soko pana la pamoja katika nchi za Mashariki na Kati ya Afrika.” Anasema Mbwiliza.

Ni fursa hizi ambazo mradi wa “Run Liemba” unaziona kwamba zinaweza kutumika kuifanya meli hii inayokaribia miaka mia moja, kuishi miaka mingine mia moja ijayo, sio tu kama meli, bali pia kama nyenzo ya mawasiliano, maingiliano na mafungamano ya kijamii, kitamaduni na kijamii.

img-20161210-wa0032

La mahusiano mema baina ya Tanzania na Ujerumani, likiwa “miongoni mwa yaliyo muhimu sana”, kama anavyosema Elisabeth Hiss, mmoja wa waanzilishi wa mradi huu.

“Dhamira ya mradi wa Run Liemba ni kuusaidia Wakfu wa Marafiki wa Liemba kufikia lengo lake. Jukumu letu ni kusaidia kuwepo kwa mashirikiano baina ya Ujerumani na Tanzani kwa kutumia mustakabali wa huduma za meli ya Liemba” Anasema Elisabeth Hiss.

Picha: Nsamila

Chanzo: DW

Comments

error: Content is protected !!