tmoja2

Mambo manne makubwa yanayolalamikiwa katika Muswada wa Habari uliopitishwa na Bunge Novemba 2016

3126
0
Share:
Share this
tmoja2

Rais wa Tanzania, Dkt Magufuli ameanza mwaka wake wa pili tangu aingie madarakani. Katika mwaka wake wa kwanza, mengi yameweza kuonekana ambayo baadhi wanayaunga mkono huku wengine wakipinga kwa sababu mbalimbali.

Katika mwaka wake mmoja aliokuwa madarakani, Rais Dkt Magufuli amejikita sana kwenye kupambana na rushwa na kurejesha nidhamu katika maeneo ya kazi hasa kwa watumishi wa umma ambao walikuwa wakilalamikiwa kila siku kutokana na huduma mbovu.
Aidha, katika kupambana na rushwa vyombo vya habari vimekuwa na mchango mkubwa sana wa kufichua maovu ya viongozi na kuwa kupambana huko na rushwa kungekuwa kugumu sana kama vyombo vya habari na waandishi wa habari wasingeshiriki.

Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari uliozua mvutano mkubwa bungeni umelalamikiwa sana na wadau wa habari kwa kuwa na baadhi ya vipengele visivyo sawa. Lakini si wadau tu waliolalamika, pia Wabunge hasa wa upinzani waliupinga muswada huu kuwa unampa Waziri mamlaka makubwa sana juu ya tasnia nzima ya habari.

Katika baadhi ya maeneo ya muswada huu ambayo yanalalamikiwa sana ni pamoja na;

Kwanza; Muswada huo haubadilishi hali iliyopo sasa ambapo serikali ina mamlaka yote juu ya vibali vya magazeti. Serikali bado itakuwa na uwezo wa kulizuia kwa muda au kulifungia gazeti lolote wakati wowote bila hata kueleza sababu ya msingi ya kufanya hivyo, au gazeti kupewa nafasi ya kujitete au Jaji wa mahakama kutoa maoni juu ya tuhuma zitakazokuwepo.

Tume ya Nyalali iliyoundwa miaka ya 1990 ilieleza kipengele hicho hakiendani na mazingira ya mfumo wa vyama vingi ulioanzishwa mwaka 1992 na pia ni kinyume na katiba ya nchi.

Pili; Katika muswada huo, Serikali imeanzisha aina mpya ya vibali kwa waandishi wa habari ambapo hakuna mwandishi wa habari atakayeruhusiwa kufanya kazi za kiuandishi wa habari hadi atakapopata kibali kutoka serikalini. Hili linalalamikiwa kwa sababu waandishi wengi watakuwa katika hatari ya kufutiwa vibali vyao pale watakapoandika masuala nyeti yanayoihusu serikali, mfano masuala ya rushwa kwa viongozi.

Tatu; Muswada huu unakandamiza uhuru wa magazeti na vyombo vingine vya habari kwa kuvipangia ni habari gani ya kuandika na namna ya kuandika habari hiyo. Katika muswada huu, vyombo vya habari binafsi vitatakiwa kuandika au kutangaza habari za serikali kutokana na muongozo utakaotolewa na serikali.

Kwa maneno mengine ni sawa na kueleza kuwa, vyombo hivyo vya habari vitakuwa vikiandika au kutangaza yale tu ambayo serikali inataka yatangazwe. Hii imeelezwa kuwa ni uvunjifu wa haki ya kujieleza inayotolewa na katiba, kwa sababu vitakosoa uwezo wa vyombo vya habari kuikosoa serikali.

Nne; Imeelezwa katika sheria za kimataifa kuwa, kumkosoa mtu hakutachukuliwa ni kumharibia heshima kama kilichoandikwa ni ukweli au ni mawazo ya mwandishi. Lakini muswada huu unaruhusu mwandishi wa habari kushtakiwa kama alichoandika kinadaiwa kumharibia mtu heshima yake hata kama ni cha kweli au kinawakilisha mawazo ya mwandishi.

Pindi muswada huu utakaposainiwa na Rais na kuwa sheria, waandishi wa habari watakuwa katika hatari ya kushtakiwa na hata kufungwa kwa sababu tu walichokiandika kimewakwaza watu wachache.Kikubwa ifahamike kuwa, uandishi wa habari ambao hautawachokonoa baadhi ya watu huo si uandishi, ni tangazo.

Jana, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liliupitisha Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 na hivyo kusubiriwa kufikishwa kwa Rais ili kusainiwa na kuwa sheria. Kwa upande wake, Rais Dkt Magufuli alisema muswada huo ukifika kwake hautachelewa hata dakika moja kabla hajausaini na kuwa sheria.

Chanzo: The Citizen

Comments

error: Content is protected !!