tmoja2

Ripoti ya uhalifu ya mkoa wa Kilimanjaro kuanzia Machi hadi Agosti

727
0
Share:
Share this
tmoja2

Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro limewafikisha mahakamani watuhumiwa 76, wakiwemo majambazi sugu kwa kuhusika na matukio mbalimbali ya ujambazi na kuvunja nyumba za watu na ofisi kwa kipindi cha Machi hadi Agosti mwaka huu.

Aidha, katika kipindi hicho zimekamatwa silaha sita, zikiwemo bastola tano na rifle moja zilizokuwa zikitumika kwa matukio ya uhalifu kwa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Wilbrod Mtafungwa alisema hayo jana katika Viwanja vya FFU Moshi mbele ya Mkuu wa Mkoa, Saidi Mecky Sadiki wakati wa hafla ya kuwapongeza askari 34 waliofanya vyema katika matukio na wajibu wao na kuliletea sifa jeshi hilo.

Kamanda Mtafungwa alisema, miongoni mwa watuhumiwa hao, 32 walihusishwa na matukio ya ujambazi na wengine 44 walidaiwa kuhusika na vitendo vya uvunjaji wa nyumba na ofisi na kuiba vitu mbalimbali vyenye thamani ya mamilioni ya shilingi.

Kuhusu dawa za kulevya, Kamanda Mtafungwa alisema watuhumiwa 555 walikamatwa na zaidi ya kilo 1,474 za bangi na mirungi na kete 131 za heroin kwa ajili ya kuuza, matumizi na usafirishaji wake kwa nyakati tofauti.

“Watuhumiwa wote walifikishwa mahakamani, sita miongoni mwao walihukumiwa kifungo cha maisha gerezani kwa kusafirisha mirungi,” alisema.

Aidha, alisema katika kipindi hicho baadhi ya matukio yamepungua na mengine kuongezeka. Alitolea mfano matukio ya ubakaji ambapo mwaka 2015 yaliripotiwa 92 huku mwaka huu yakiwa 151 na ulawiti mwaka 2015 yalikuwa saba huku mwaka huu yakiwa 12.

Alisema pamoja na hilo, matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha yamepungua kutoka 29 mwaka 2015 hadi 18 mwaka huu, unyang’anyi wa kutumia nguvu umepungua kutoka 104 mwaka 2015 hadi 96 mwaka huu na uvunjaji wa nyumba kutoka matukio 177 hadi matukio 74 mwaka huu.

Alisema mafanikio hayo yanatokana na kazi nzuri ya askari kwa ushirikiano na raia wema na wadau wengine ambao kwa namna moja au nyingine huvisaidia vyombo vya dola. – HabariLeo

Comments

error: Content is protected !!