tmoja2

Taarifa kwa waliokuwa wakisubiri kupangiwa vituo vya kazi kabla ya ajira kusitishwa serikalini

488
0
Share:
Share this
tmoja2

Sekretarieti ya Ajira ya Utumishi wa Umma imesema kuwa watu wote walioomba ajira na wakawa wamefanyiwa usaili na kufaulu lakini kabla ya kupangiwa vituo vya kazi ajira zikasitishwa watatakiwa kuomba tena mara ajira zitakapotangazwa.

Mamlaka hiyo inayohusika na kuajiri watumishi wa umma iliyasema hayo ilipokuwa ikijibu swali na kueleza kuwa kama zoezi la usitishwaji ajira litazidi kipindi cha miezi sita tangu usaili ilipofanyika, waombaji watatakiwa kuomba upya ajira zikitangazwa.

Kwa maana nyingine ni kwamba kama zoezi la usitishwaji ajira halitazidi miezi sita tangu usaili ulipofanyika, wale waliofaulu usaili wataweza kupangiwa vituo vya kazi ajira zikitangazwa.

Sekretarieti walikuwa wakijibu swali hili kupitia mtandao wao;

Swali la 2.

Hivi mtu ambaye alifanya usaili wa ajira za utumishi wa uma na alikuwa anasubiri matokeo ya usaili, kabla matokeo kutoka ajira zikasitishwa ,je mkianza kuajiri ataajiriwa kwa usahili huo ?

Jibu

Tunashukuru kwa swali lako, Ni kweli Serikali ilisitisha kwa muda mchakato wa ajira mwezi juni kwa ajili ya kupisha zoezi linaloendelea la watumishi hewa, Aidha endapo zoezi la kusitishwa kwa ajira halitazidi kipindi cha miezi sita tangu usaili ulipofanyika na endapo ulifanya usaili na ukawa umefaulu ajira zikifunguliwa unaweza kupangiwa kituo cha kazi na kuajiriwa. Sekretarieti ya ajira ina utaratibu wa kuhifadhi kwenye kanzidata waombaji kazi waliofaulu ambayo hudumu kwa kipindi cha miezi sita (6) kwa mujibu wa Kanuni za Uendeshaji za Sekretarieti ya Ajira.

Maswali mengine yaliyoulizwa na kujibiwa na mamlaka hiyo unaweza kuyasoma hapa;

Swali la 1

KUHUSU UTARATIBU WA KUFUATA ILI KUREJESHWA KAZINI.

Husika na kichwa cha habari hapo juu, mimi ni mmoja kati ya wale walio fanya usaili mwezi Septemba 2015 na kufaulu kisha kupokea barua ya kupangiwa kituo cha kazi kwa Cheo cha Afisa maendeleo ya jamii Daraja la Pili. Hata hivyo baada ya kukamilisha usajili ikiwa ni pamoja na kujaza fomu ya mkataba jina langu halikuingizwa katika orodha ya malipo (payroll) na baada ya kufuatilia nilipata taarifa kuwa cheti changu cha (higher diploma) hakikutambuliwa katika scale za mishahara hivyo nilipaswa kurejea chuo ili kupata cheti chenye rank zinazo tambuliwa ndipo nirejeshwe kazini kama kawaida. Sasa nimemaliza masomo na nina Degree ya maendeleo ya jamii, Naomba kurejeshwa kazini kulingana na makubaliano ya awali na naomba nipewe utaratibu wa kufuata ili kufikia hatua hiyo.

Jibu lolote litanipa Mwanga ktk harakati za kimaendeleo ndani ya Taifa langu, natarajia busara toka kwako katika kutatua tatizo langu,

Jibu

Hongera kwa kufaulu na kupangiwa kituo cha kazi. Pamoja na hilo tunakupa pole kwa kutoweza kuingia katika orodha ya wanaolipwa mishahara na Serikali kama ambavyo umeeleza. Kwa jinsi ulivyotoa maelezo yako tunaweza kukushauri kufanya yafuatayo:-

i. Waajiri wote waliopo katika Serikali huajiri watumishi kwa kila kipindi cha mwaka mmoja wa fedha endapo watapewa kibali na kukifanyia kazi katika muda uliopangwa na si vinginevyo. Hivyo si rahisi mwaka husika utakapopita bila kutekeleza ajira hizo kuweza kuendelea nazo, vinginevyo kuwepo na ruhusa ya kufanya hivyo kutoka katika Mamlaka husika.

ii. Kwa kuwa sasa umekwishafanikiwa kupata Shahada ya Maendeleo ya Jamii ni vema ukiona matangazo ya kazi yanayohusiana na kada hiyo na kukidhi vigezo uombe kazi ili uweze kuajiriwa.

iii. Kwa kuwa ajira yako ilishapitiliza mwaka bila ya kukamilika kama ulivyoeleza si rahisi kuendelezwa kutokana na taratibu za muda wa utekelezaji wa vibali vya ajira ambavyo huwa ni ndani ya miezi mitatu tangu tarehe ya kuidhinishwa.

Tunakushauri kuendelea kutembelea tovuti ya Sekretarieti ya ajira kwa ajili ya kuona matangazo ya fursa za ajira zilizopo na maeneo ya waajiri wengine kama tulivyoshauri.

Swali la 3

Habari za kazi mheshimiwa na pole kwa majukumu ya kulijenga Taifa.

Ninaomba kuishauri serikali kupitia upya ama kutunga sheria mpya ili kulinda maslahi ya sisi wazawa na Taifa kwa ujumla, kama ifuatavyo;

1. Baadhi ya wawekezaji wachache si wengi, hawatoi mikataba ya kazi kwa wafanya kazi kama sheria ya ajira inavyoelekeza na mfanya kazi akihoji kuhusu hili ananong’onezwa kuwa hiyo ni njia ya kupunguza watu wakati mfanya kazi anatimiza wajibu wake. Tatizo hili lipo sana kwa baadhi si  wote, wawekezaji wenye asili ya asia hasa India.

2.Baadhi ya wawekezaji hasa wenye asili ya asia hawatoi bima ya afya kwa wafanya kazi kama sheria mpya ya kazi inavyoelekeza waajiri kufanya hivyo.

3.wawekezaji wengi 90% , wamegeuza nchi yetu kama shamba la bibi, kwa kulipa mishahara duni, ya kinyonyaji bila kuzingatia ujuzi au kiwango cha elimu alichonacho mfanya kazi. hapa sijui kama hili tatizo ni la wizara kwa kutotoa muongozo wa malipo ya mishahara kwa kuzingatia elimu ya mfanyakazi au la?. mimi si mwanasheria.

graduate amemaliza masters degree ,engineering analipwa laki nne(400,000) sawa na gate man , hata ukiwa na phd , the same payment  but mfanya kazi mwenzio mwenye certificates ambaye anatoka nchi ya muwekezaji , hana experience , anachofanya na wewe hicho hicho , analipwa milioni ishirini(20,000,000) Tzsh.

Serikali inakosa mapato kupitia makusanyo hafifu ya kodi, wasomi wataendelea kukwepa kurudisha mikopo helseb kwakua laki nne hata wao haziwatoshi na hakuna kazi lazima wafanye wasirudi geita. nijitolee mfano mimi niliacha kazi viettel now halotel last year for this neo- colonialism exploitation under the umbraler  of investment.

my take: serikai itunge sheria kwa wawekezaji kulipa mishahara elekezi kama wafanya kazi wa serikali wanavyo lipwa na haki zote pia, maana watanzania wote hatuwezi kufanya kazi serikalini. Kama wizara itafanya hivyo, naamini kabisa , hakutokuwa na wadaiwa sugu wa bodi ya mikopo , kodi kubwa itakusanywa na nchi itasonga mbele bila kumpigia magoti tapeli yoyote mweupe. Naamini serikali sikivu na ya kizalendo ya hapa kazi tu, hili inaweza kulitekeleza. nakutakia kheri katika ujenzi wa Taifa.

Kind regards;

Jibu

Tumepokea maelezo ya swali pamoja na maoni yako. Hata hivyo tungependa kukushauri kuwa kuwa suala la mikataba ya ajira na kima cha chini cha mishahara kwa Taasisi binafsi (Private sectors) linashughulikiwa na Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na watu wenye Walemavu. Hivyo ni vema suala hili likaelekezwa katika ofisi hiyo ili liweze kujibiwa ipasavyo.

Swali la 4.

AJIRA YANGU YA AFISA USHIRIKA DARAJA II-WILAYA YA KITETO

Ndugu Katibu Mkuu, Husika na kichwa cha habari hapo juu. Mnamo Septemba mwaka jana nilifanya usaili mara mbili yaani kwa kuandika na kwa mahojiano ya kazi ya Afisa Ushirika. Baada ya interview zote mbili tuliambiwa tusibirie baada ya mwezi tutapata majibu kama tumepata kazi au la.

Mnamo November 2015 yalitoka majina ya watu na vituo vyao vya kazi lakini kwenye orodha hiyo jina langu halikuwepo. Baadae mwezi Machi, 2016 nilipigiwa simu kutoka Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma niende kuchukua barua ya kuajiriwa. Nilienda kuichukua barua ile na nikawa nimepata ajira kama Afisa Ushirika Daraja II katika Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto. Nilienda kuripoti kwenye kituo changu cha kazi. Nilipofika pale nilielezwa kwamba serikali imesisitisha ajira za watu wote waliokuwa wameajiriwa mwaka 2016 na kutakiwa kurudi nyumbani hadi itakapowaita. afisa utumishi wa Wilaya ya Kiteto akaniambia kwa kuwa serikali imesistisha ajira hawezi kunipokea hadi hapo tangazo la kuwarudisha wale waliokuwa wamesimamisha litakapotoka ili miweze kuripoti. Sasa ndugu Katibu Mkuu kwa hali yangu kama hii nifanyeje? na je serikali ishatoa waraka wa kuwarudisha kazini watumishi waliojiriwa mwaka huu ambao walipisha zoezi la uhakiki wa watumishi hewa?

Naomba mwongozo wako

Jibu

Pole sana Bw. Gwawilo kwa usumbufu utakaokuwa umeupata. Ni kweli kama ulivyoeleza Serikali ilisitisha ajira mnamo mwezi Juni, 2016 kwa ajili ya kupisha zoezi la uhakiki wa watumishi hewa, Aidha kwa kuwa tayari ulishapewa barua kwa ajili ya kwenda kuripoti kwa mwajiri wako huko Kiteto tunakushauri uendelee kuwasiliana na mwajiri wako ulipopangiwa kwa ajili ya kupata mrejesho na maelekezo zaidi kwa kuwa Sekretarieti ya Ajira ilikwisha kamilisha kazi ya kukupangiwa kituo cha kazi.

Swali la 5.

Hongereni sana kwa kazi mnazofanya. Samahani naomba kujua jambo moja. Mwezi mei vijana takribani 3000 waliajiriwa lakini mwezi June ajira zao zilisitishwa. Sasa kuna taarifa kuwa ajira zile zimefutwa na vijana wale watapaswa kuomba upya pindi ajira zitakapo tangazwa. Je kuna ukweli juu ya jambo hili?

Jibu

Asante kwa swali na tunashukuru kwa pongezi zako. Mpaka sasa Sekretarieti ya Ajira haijapokea taarifa ya kufutwa kwa ajira ulizozitaja, Serikali ilisitisha ajira mpya mwezi Juni mwaka huu kwa ajili ya kupisha zoezi la uhakiki wa Watumishi hewa na mara baada ya zoezi hilo kukamilika na kuanza mchakato wa Ajira kwa kada mbalimbali mamlaka husika zitatoa taarifa kamili ikiwa ni pamoja na waombaji kazi ambao walisharipoti kazini na kusitishiwa ajira zao.

Swali la 6.

Habari za kazi,kwanza nitangulize shukurani zangu za dhati kwa utendaji kazi wenu, mimi nifanya usaili chuo cha ardhi wa maandishi na baadae usaili wa mahojiano, baadae Mh rais akasitisha ajira .Nilikuwa nataka kujua kama mchakato ulishamalizika ama bado tuendelee kusubiri. Ahsante

Jibu

Tunashukuru kwa pongezi zako na tumepokea swali lako, tunapenda kukujibu kuwa kwa sasa zoezi la uhakiki bado linaendelea na litakapokamilika taarifa kamili itatolewa na Mamlaka zinazohusika kwa hatua inayofuata.

Swali la 7.

Poleni sana na kazi na hongereni kwa kazi nzito mnayoifanya kwa mafanikio makubwa! Nilipitia moja ya majibu ya hoja za wadau za mwezi oktoba kwa swali ambalo kuna mtu aliuliza kuhusu majina ya watu waliokua wamehifadhiwa kwenye kanzidata juu ya usalama wao kutokana na ajira kusitishwa! Katika majibu yenu mlisema majina yanahidhiwa kwa muda wa miezi 6 hivyo sababu ajira zilisitishwa mwez june ikifika mwezi desemba majina hayo yataondolewa! Maoni yangu ni kuwa kwanini watu hawa wasiendelee kuwepo kwenye kanzi data sababu ajira zimesitishwa ivo kuwaondoa kwenye kanzidata wakati ajira bado hazipo naona kama hawatendewi haki, ombi langu ni kuwa naomba mliangalie swala hili kwa mara ya pili tena ili watu hao walio kwenye kanzi data wasiondolewe mpaka ajira zitakaporuhusiwa hata yakikaa kwa mwezi mmoja tu baada ya ajira kuruhusiwa! Nitoe shukrani zangu tena kwa mara nyingne niwatakie utendaji mwema wa kazi naamini ombi langu kitapokelewa na kufanyiwa kazi.

Jibu.

Asante na hongera kwa kutufuatilia kwa ukaribu. Kwa mujibu wa Taratibu zetu za uendeshaji wa mchakato wa ajira majina ya waombaji kazi waliofaulu lakini hawakupangiwa vituo vya kazi kwa sasa huhifadhiwa kwenye kanzi data kwa muda usiozidi miezi sita, Aidha ushauri wako tumeupokea na tunaufanyia kazi kadiri itakavyowezekana.

Swali la 8

Habari za kazi,pole na majukumu ya kazi, kwanza nashukuru sana kwa kunipangia nafasi ya kazi baada ya kufaulu interview. Nilirepot kituo cha kazi tangu mwezi wa nne(4) mwaka huu (2016) nasikitika kabla sijapata check number tangazo la kusitisha ajira likatoka,lakini kuna wengine ambao walipata tukio nzuri la kupata check number kabla ya kusitishwa ajira.

Sababu napenda sana nafasi hii nimeendelee kuwa mvumilivu nikiwa kituo cha kazi mpaka pale nitakapoingizwa kwenye payroll.  kwa wale waliokuwa wamepata check number  nakusitishwa mshahara wao kuna tamko linaloonyesha kwamba mwezi huu warudishwe tena kwenye system natumai wataanza kupata mshahara.  Naomba msaada wenu angalau kujua na mimi nitaingizwa wakati gani kwenye payroll angalau na mimi nianze kupata mshahara. muwe na kazi njema na siku njema pia.

Jibu

Asante kwa swali lako. Ni kweli ajira zilisitishwa ili kupisha zoezi la uhakiki wa watumishi hewa ambalo linaendelea, Tunachokuomba kuendelea kuwa mvumilivu hadi hapo mamlaka husika zitakapotoa taarifa za kukamilika kwa zoezi hilo. Aidha kwa kuwa tayari ulishapangiwa kituo cha kazi tunakushauri kuendelea kuwasiliana na Mwajiri wako kwa ajili ya taarifa zaidi kuhusu ajira yako.

Swali la 9.

Ndugu Mheshimiwa, salam, Naomba kujua kuhusu swala hili: Je uhakiki utakapokamilika, Sekretarieti ya ajira itatangaza tena upya zile nafasi za kazi zilizokuwa zimetangazwa na taasisi za serikali ule mwezi wa tano kabla ya zoezi la uhakiki kuanza? Kwakuwa ajira za serikalini zilisitishwa kwanza kwaajili ya zoezi la uhakiki lililoanza tangu mwezi wa sita, kwa mfano Chuo kikuu cha dar-es-salaam kilitangaza nafasi za kazi mwezi wa tano na nyingine mwezi wa saba, je sekretarieti ya ajira itarudia kuzitangaza nafasi zile? Au utaratibu utakuwaje?

Jibu

Tunashukuru kwa swali lako, Kwa mujibu wa kumbukumbu zetu nafasi hizo zilizotangazwa na Chuo kikuu cha Dar es salaam hazikutangazwa kupitia sekretarieti ya ajira hivyo ni vizuri kuwasilisha swali lako chuo husika kwa ajili ya majibu ya kina.

Swali la 10

Habari za kazi mkuu, naomba kuuliza sisi tulioajiriwa mwezi mei na hatukupata mshahara tutarudishwa lini kazini?maana wenzetu waliopata walau mshahara mmoja wameitwa.Asante natumaini swali langu litajibiwa.

Jibu

Ni kweli wapo baadhi ya waombaji kazi ambao walifanya usaili ambapo wale ambao walifaulu walipangiwa vituo vya kazi kwa waajiri mbalimbali kabla ya kusitishwa kwa jili ya kupisha zoezi la uhakiki wa watumishi hewa Serikalini. Aidha kwa kuwa tayari ulishaajiriwa kabla ya usitishwaji wa ajira hiyo tunakushauri uendelee kuwasiliana na mwajiri wako kuhusu ajira yako kwa kuwa Sekretarieti ya Ajira ilishamaliza kazi yake.

Swali la 11.

Habari, Hongereni kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya katika kuhakikisha wananchi wa kitanzania wanapata ajira bila kuwepo na upendeleo au rushwa ya aina yeyote ile. Napenda sana kuipongeza sekretarieti ya ajira katika utumishi wa umma. Mwenyezi Mungu awabariki sana. Baada ya pongezi zangu nilipenda kutaka kufahamu mwenendo wa ajira mpaka sasa unavyoenda. Kama sijakosea mnamo tarehe 04/11/2016 Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimu Dr. John Pombe Joseph Magufuli akiwa Ikulu alipata nafasi ya mahojiano na waandishi wa habari lengo likiwa kufafanua na kuuelezea umma juu ya utendaji wake wa kazi baada ya kumaliza mwaka wake wa kwanza toka achaguliwe kuwa rais. Moja ya maswala aliyotolea ufafanuzi ni pamoja na ajira. Mheshimiwa Rais alisema kuwa swala la ajira kusimamishwa halipo tena na ajira zimeendelea kutoka katika taasisi tofauti za umma ikiwemo Wizara ya Afya.Sasa naomba kuuliza mbona hamtangazi ajira na ikiwa Rais ameshasema ajira zinatolewa kwa sasa huku uhakiki wa watumishi hewa ukiendelea? Ningefurahi endapo swali langu mngenijibu kwa kunipatia maelezo. Nashukuru sana na Kazi njema.

Jibu.

Tunashukuru kwa pongezi zako. Tunaomba kukufahamisha kuwa nafasi hizo za wizara ya Afya, hasa kwa kada za madaktari na wauguzi mchakato wake wa ajira haupitii Sekretarieti ya Ajira kama nafasi hizi husimamiwa na kuratibiwa moja kwa moja na wizara husika. Aidha kwa nafasi za kazi zinazopitia sekretarieti ya Ajira zinatangazwa baada ya kupata kibali/vibali vya Ajira toka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi Wa Umma na Utawala Bora, kwa nafasi ambazo tumekuwa tukipata vibali zimeendelea kutangazwa kadri zinavyojitokeza.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma,

27 Barabara ya Bibi Titi Mohamed,

S.L.P 63100,

Maktaba Complex,

11102 Dar es Salaam

Comments

error: Content is protected !!