tmoja2

Tafakuri ya Jumapili: Kwaheri Castro

206
0
Share:
Share this
tmoja2

Fidel Alejandro Castro Ruz, maarufu Fidel Castro ni Mwanamapinduzi na Mwanaharakati wa haki za Kijamii Amerika ya Kusini na dunia nzima ya nchi za Kusini. Kwake cheo hakikuwa na maana yoyote zaidi ya nafasi ya kutumikia wanaoonewa. Waziri Mkuu (1959 -1976) na Rais wa Cuba (1976 -2008), alizaliwa mwaka 1926 na kufariki wiki hii tarehe 25 Novemba, 2016. Hayati Fidel Castro ameondoka katika uhai wa mwili kama ambavyo kila binadamu atafanya hivyo, lakini kwa hakika atabaki katika kumbukumbu za kihistoria (kama alivyosema katika hotuba yake ya utetezi mahakamani 1953, “History will absorb me”) za marafiki na maadui zake kwa miaka mingi ijayo – ilimradi dunia inaendelea kuwepo na binadamu wakiendelea kuwa sehemu ya viumbe hai katika sayari hii (kwa mipango ya Mungu.

Historia inaonesha kuwa alikuwa mtukutu na mtu mwenye misimamo isiyoyumba kiasi cha wakati fulani kufukuzwa shule. Tunachoweza kujifunza hapa ni uwepo wa vinasaba vya uasi dhidi mifumo na mambo aliyoyaona kuwa kinyume cha haki.  Lakini harakati katika azma ya kutetea haki za kijamii zilianza kufahamika akiwa mwanafunzi wa sheria katika chuo kikuu cha Havana ambapo alijaribu kugombea bila mafanikio urais wa serikali ya wanafunzi. Alijunga na siasa na kugombea uwakilishi mwaka 1952 lakini kabla ya uchaguzi serikali ilipinduliwa na dikteta Fulgencio Batista ambaye alipiga marufuku siasa za kidemokrasia na kikatiba. Yeye pamoja na  wenzake hawakukubali wakaamua kuanzisha kikundi cha kiharakati kwa jina “The Movement” na baadaye kufanya jaribio la mapinduzi kwa kuvamia kambi ya jeshi Mancada, Julai 26, 1953. Jaribio lillishindwa ambapo Castro, mdogo wake Raul (Rais wa sasa wa Cuba) na wanamapinduzi wengine  walihukumiwa miaka 15 jela katika kisiwa cha Pines.

Ushahidi wa kihistoria unaonesha jela huwa si mbinu nzuri sana ya kuzima azma, ari na dhamira ya wanaharakati wa kisiasa wanaopambana kwa haki (Just causes) na kwa ajili ya masilahi ya wengi. Mbinu nzuri huwa ni kutafuta majawabu sahihi ya sababu zinazowazalisha wanaharakati hao.  Mifano ni mingi,  kuanzia Adolf Hitler (Dikteta mbaya kuliko wote katika karne ya 20) aliyetumia muda wake akiwa  jela kuandika mawazo  pamoja kitabu chake cha My struggle kilichokuja kuwa msingi wa umaarufu wa chama chake cha Nazi. Mwingine ni Malcom X, Mwanaharakati wa haki za watu weusi nchini Marekani aliyefungwa jela (si kwa kosa l kiharakati) miaka 8 lakini alitumia muda akiwa jela kusoma kila kitu, alipotoka hakuwa anazuilika hadi aliponyamazishwa na wabaya wake kwa risasi mwaka 1965. Mfano mwingine ambayo ni rahisi kwa hapa kwetu Afrika ni Rais Robert Mugabe aliyefungwa na serikali ya Ian Smith na  Nelson Mandela,  aliyetumikia kifungo kaika jela ya  makaburu kwa miaka 27 – alipotoka alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa Afrika kusini huru.

Kwa hiyo,  kwa Castro pia kifungo kilimpa nafasi nzuri ya kutafakari, kusoma vitabu kama vile vya Karl Marx na Lenin na kuandika makala ambazo ziliendelea kuhamasisha umma wa wana Cuba na wanaharakati kuelewa vyema dhamira na haja ya kile walichokisismamia. Bahati nzuri waliachiwa huru kwa msamaha wa Batista baada ya miezi 22 na kuamua kuhamia nchini Mexico kupanga vizuri mapinduzi kupitia kikundi chao “The Movement” ambacho kilibadilishwa jina kuitwa “The 26th of July Movement” kuenzi jaribio la mapinduzi katika kambi ya jeshi ya Mancada na waliopoteza maisha katika tukio hilo. Lilifanyika tena jaribio la pili mwaka 1956 baada ya kurejea Cuba kutoka Mexico. Hawakufanikiwa kwa mara nyingine na wengi wa waasi wakapoteza maisha. Waliobaki akiwemo Castro, mdogo wake Raul na Ernesto Che Guevera, maarufu kama “Che”  walikumbilia milima ya Sierra Maestra kujificha na kujipanga kwa ajili ya vita vya misituni. Hawakuwa tayari kusaliti shabaha. Baadhi ya wanahistoria wanaeleza kuwa serikali ya Fulgencio Batista iliamini kwamba Fidel Castro alikufa katika uvamizi huo. Pamoja na kwamba maisha ya Sierra Maestra yalikuwa magumu sana lakini kwao shabaha ilikuwa zaidi ya kitu chochote; ilikuwa ni zaidi ya njaa ya chakula, ilikuwa ni zaidi ya fikra ya kuishi au kupoteza maisha na, kwa Castro, ilikuwa juu hata ya ukweli kwamba familia yake ilishasambaratika baada ya mke wake kumuacha. Bahati nzuri wakulima masikini waliochwa na serikali na waliochoswa na hali mbaya na siasa za maslahi ya makundi na magenge ya walaji, waliwasaidia kwa namna walivyoweza. Hatimaye seriakali ya Batista iliendelea kujimaliza yenyewe kwa rushwa na uonevu kiasi cha kuifanya Marekani iliyokuwa inawapa misaada mbalimbali ikiwemo ya kijeshi kujiondoa. Pia kuongezeka kwa upinzani wa ndani dhidi ya serikali kulisaidia kuhitimisha harakati za Sierra Maestra kwa mapinduzi ya tarehe 1 Januari, 1959.

Hayati Castro alianza kuongoza Cuba akiwa Waziri Mkuu ambapo aliweka bayana kuwa shabaha ya mapinduzi haikuwa juu yake kutawala bali kuhakikisha wananchi wanamiliki nchi yao na kutawala mustakabali wao. Utekelezaji wa shabaha ya mapinduzi ulianza mara moja kwa mageuzi katika kilimo, afya na elimu na huduma mbalimbali za kijamii. Serikali ilianza kupanga na kuratibu kilimo cha kisasa kwa kupokonya ardhi na mashamba makubwa wale waliohodhi na kuwagawia wananchi masikini ambapo shamba la kwanza kupokonywa na serikali lilikuwa shamba la familia yake Castro. Mama yake Castro, Lina, hakupenda – lakini kwa Castro, shabaha ilikuwa bora kuliko masilahi binafsi ya familia yake.   Mageuzi makubwa yaliyofanyika katika sekta mbalimbali zilisaidia kwa haraka sana wananchi  kuielewa na kuimiliki shabaha ya mapinduzi.

Nimesema Fidel Castro si rahisi hata kidogo kusahaulika katika historia. Aliweza kuongoza harakati zilizotoa taswira ya ukombozi kwa upande mmoja na tishio la uwepo kwa upande mwingine kwa wakati mmoja. Kwa Cuba, Amerika ya Kusini na Afrika au dunia iliyochoka unyanyasaji na unyonyaji, alionekana kama alama ya ukombozi na upinzani wa kweli dhidi ya mifumo dhalimu ya dunia. Kwa upande mwingine aliifanya nchi ndogo, Cuba,  iliyopo umbali wa maili 90 kusini mashariki mwa Marekani kuwa tishio kwa mfumo wa maisha na usalama  kiasi cha kukaribia kuleta maangamizi ya kisiwa kidogo katika Caribbean.

Marekani haitaisahau mwaka 1962, ambapo Fidel Castro kwa msaada wa serikali Sovieti chini ya Waziri Mkuu Nikita Khrushchev, aliamua kuyasimika makombora ya nyukilia akiyaelekeza Marekani katika kile ambacho wachambuzi wanaona kama jaribio la mwisho la kuyalinda mapinduzi ya Cuba dhidi ya Taifa lenye nguvu duniani. Marekani haikupenda hatua za kijamaa zilizochukuliwa na serikali ya Cuba ikiwa ni pamoja na kutaifisha makampuni, mashirika na mali zilizomilikiwa na wamarekani na hasa ukaribu wake na Sovieti. Serikali ya Marekani iliamua kuiwekea vikwazo vya kibiashara na baadaye kusitisha uhusiano wa kidiplomasia mwaka 1961. Marekani ilifanya majaribio mengi ya siri na ya wazi kutaka kumuondoa Fidel Castro lakini zote zilishindwa. Kubwa ni ule uamuzi wa Rais John Kennedy kukubali ndege za Marekani zitumike kusaidia waasi katika jaribio la mapinduzi katika uvamizi maarufu kama “Bay of Pigs”.  Uvamizi ulishindwa  baada ya majeshi ya Castro kuyazima kama moto wa mshumaa. Ilikuwa aibu kubwa kwa serikali ya Rais John Kennedy mbele ya dunia na mbele ya wananchi wa Marekani ambao kama wangejua wasingekubali hata kidogo.

Hata hivyo, Rais Kennedy baada ya aibu ya “Bay of Pigs” alichukua tahadhari juu ya ushauri anaopewa na wasaidizi wake wakiwemo majenerali juu ya kuchukua hatua za kijeshi baada ya kugundulika kwa makombora ya nyukulia. Busara ya Kennedy ya kuamua kuiweka pembeni fahari ya Marekani na kuamua kuwasiliana na Waziri Mkuu wa Sovieti, Nikita Khrushchev, uliiondoa dunia katika uwezekano wa vita ya nyuklia. Kwa mujibu wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, pamoja na wanahistoria mbalimbali, mgogoro wa makombora ya Cuba uliisha baada ya Rais Kennedy na Khrushchev kukubaliana kwamba Marekani haitaivamia tena Cuba. Sovieti iliondoa makombora na Marekani haikuwahi tena kutaka kuivamia Cuba. Inaelezwa kuwa Rais Kennedy alikasirika kiasi kwamba hakutaka kusikia pendekezo lolote litakaloliweka Marekani na Sovieti katika hali ya vita kama ile. Hata hivyo, Marekani iliendelea na  mipango ya siri dhidi ya Castro ambayo yote yalishindwa hadi alipoachia madaraka mwaka 2008.  Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Marekani na Cuba ulirejeshwa na Rais Barack Obama mwezi Julai mwaka jana baada ya miaka 54.

Sababu kubwa ya Marekani kuingilia Cuba ilikuwa ni wasiwasi, kama ilivyodokezwa na Mwanadiplomasia wa zamani wa Marekani aliyeongoza kitengo cha msalahi ya Marekani Cuba, Wayne Smith.  Kwanza, kwamba Cuba ingeweza kutumika na Sovieti na hivyo kuhatarisha usalama wa Marekani. Pili, kwamba kama mapinduzi yangefanikiwa yangekuwa kigezo kichochezi katika Amerika ya Kusini hivyo kusambaa kwa mawazo ya Kikomunisti na ushawishi wa Sovieti.

Kwa vyovyote vile,  hatua zilizochukuliwa na Marekani hazikufanikiwa kwa sababu dunia nzima haikuona Cuba katika jicho la uhasama kama baadhi ya viongozi wa Marekani walivyotaka ionekane. Kama kuna kitu uhasama huo umekifanya ni kumjenga Fidel Castro na nchi ya Cuba kuwa shujaa na kinara katika siasa za dunia na hasa dunia ya tatu au nchi zinazoendelea, maarufu kama “Nchi za Kusini”. Kwa Amerika ya Kusini naamini watu aina ya Marehemu Hugo Chavez wa Venezuela na Rais Ivo Morales wa Bolivia na wengine wengi ni zao la mafanikio ya Castro dhidi ya mfumo wa kidunia unaonyonya nchi masikini.

Kwa hakika niungane na Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Thabo Mbeki kwamba Fidel Castro hatasaulika katika harakati za ukombozi wa Afrika. Mchango wake katika ukombozi wa Afrika ukiwemo wa Angola ambapo wanajeshi wa Cuba walishiriki moja kwa moja kumwaga damu dhidi ya  majeshi ya makaburu ni alama isiyofutika. Ulikuwa raia wa Cuba kwa hati ya kusafiria,  lakini kwa moyo ni mwafrika na ni raia wa dunia pia. Kwaheri Fidel Castro, Shujaa wa Sierra Maestra.

Alex Manonga

Maoni: +255717162436

Comments

error: Content is protected !!