Header Ad

zinazosomwa zaidi

Most Viewed

Agizo la DC Bariadi la kuwataka watumishi kununua mashine ya ultrasound latenguliwa

Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini ametengua agizo la Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga la kuwataka watumishi 137 wa Hospitali ya Mji wa Bariadi kuchanga TZS 30 milioni ili kununua mashine mpya ya ultrasound kufuatia iliyokuwepo kuibwa.

DC KIswaga alitoa agizo hilo jana Agosti 14, ikiwa ni siku moja baada ya kuripotiwa kuibwa kwa mashine hiyo ambayo ilikuwa ikitumiwa na wazazi.

Akitengua agizo hilo RAS Sagini amesema kuwa ni lazima mwizi apatikane na awajibishwe, na si kuchangisha wasiohusika.

Amesema kuchangisha watumishi wote sio sahihi kwani kuna wengine walikuwa likizo, na hivyo watakuwa wanaingizwa kwenye tukio ambalo pengine hawahusiki.

Amesema serikali inavyo vyombo vya uchunguzi, na tukio hilo ni moja ya kazi ya vyombo hivyo, ambapo ameliagiza Jeshi la Polisi kuanza uchunguzi mara moja, na mhusika atakapobainika atachukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Mike Mabimbi, alisema mashine hiyo iliibwa Agosti 5 mchana, mwaka huu na hadi sasa haijapatikana.

Mabimbi alisema baada ya kutokea tukio hilo, walitoa taarifa polisi na watu 17 wakiwamo wauguzi walikamatwa kwa mahojiano.

Alisema baada ya kuibwa kwa kifaa hicho, wanalazimika kuwapeleka kina mama wajawazito katika mashine kama hiyo kubwa iliyoko chumba cha mionzi, takribani mita 10 kutoka wodi yao na kueleza kuwa inasababisha usumbufu.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Mwanaidi Churu, alisema mazingira ya kuibwa kwa kifaa hicho yameendelea kuwa magumu kutokana na watoa huduma katika wodi hiyo waliokuwepo siku hiyo kila mmoja kudai hajui.

Bitnami