Header Ad

zinazosomwa zaidi

Most Viewed

Fahamu aina mbalimbali za madini yanayopatikana Afrika, na matumizi yake

Kila mtu anafahamu kuwa dunia kuna madini, tena ni moja ya bidhaa zenye thamani sana, ambapo maelfu ya watu na kampuni zimeweza kupata utajiri kupitia bidhaa hizo.

Lakini wengi wetu mbali na kujua uwepo wa madini, hatujui matumizi yake. Kwamba mtu anayenunua mfano Almasi, huwa anakwenda kufanya nayo nini?

Makala hii ina lengo la kukuelezea kwa ufupi aina mbalimbali za madini zinazopatikana nchini Tanzania na nchi jirani pamoja na matumizi yake. Uchambuzi huu wa matumizi ya madini ulitolewa kupitia mtandao wa Twitter na mtumiaji Pat Nanyaro

ALMASI: Moja kati ya madini ya vito yenye thamani sana. Hutumika kama urembo na pia katika kukatia vitu vigumu sana kama chuma (steel), vioo na kuchorongea miamba migumu. Hii ni kutokana na ugumu wake wa kupindukia.

Almasi yote ikiisha bado tutapata almasi mpya kwani wanasayansi wamegundua namna ya kutengenza almasi Maabara kwa kutumia joto la juu sana na mshinikizo mkubwa! Usistaajabu. Almasi inaweza pikwa, sio kuchimbwa pekee!

TANZANITE: Madini haya ya vito yenye rangi ya bluu yakikatwa na kuokwa, hupatikana Tanzania pekee (kwa mujibu wa taarifa tulizo nazo). Madini haya yaligunduliwa kama zali tu wakati watu wanatafuta Ulanga (ule wa kwenye betri au penseli).

Ukiondoa kutumika kwenye vidani na kwingineko, Tanzanite ndio kito chenye ugumu zaidi ukiondoa Almasi. Na mara nyingi imekuwa ikitumika katika shughuli ambazo zingehitaji Almasi kama kukata vioo, miamba n.k.

ULANGA: Kwa kimombo Graphite. Madini haya tunayajua zaidi kwenye penseli, lakini pia ukibomoa betri utaona unga mweusi. Hivi majuzi imegundulika kuna mashapo makubwa ya Ulanga katika maeneo ya Mererani, Lindi na huko Morogoro.

Kutokana na wingi huo wa Ulanga ni dhahiri Tanzania inaweza kuwa na nafasi ya pekee duniani kwani kukua kwa teknolojia ya nishati mbadala inayotumia betri inaweza kukuza uhitaji wake. Pia wawe makini kuchekecha, jiolojia ya ulanga inaruhusu uwepo wa vito kama almasi/tanzanite. Duru za kisayansi pia zinasema ukichukua kipande cha ulanga ukakiweka kwenye mazingira ya joto na shinikizo kubwa sana, kinaweza kugeuka kuwa ALMASI! (Rudi hapo juu kwenye Almasi ya Kutengeneza). Hii ni kutokana na muundo wa kikemikali unaokaribiana sana kati hizi mbili.

KOBALTI: Madini yanayopatikana Kongo ya Kabila kwa wingi kuliko kwingine Afrika na ni kati ya nchi chache duniani zenye jiolojia yenye madini hayo. Moja kati ya vyanzo vya migogoro isiyoisha kwa majirani zetu.

Kukua kwa teknolojia ya magari ya umeme (wakina Tesla) na matumizi ya umeme jua vinategemea sana madini haya. Thamani na umuhimu wake hata hivyo haujawahi onekana kwa Wakongo, kelele za Ajira kwa watoto, umaskini, vita na madhara ya kiafya huzidi faida tarajiwa.

FEDHA: Dhahabu ni ya Mwanamke, Ilhali Fedha huvaliwa na Mwanaume! (Usiulize nimejulia wapi). Mapacha hawa kama ilivyo katika matumizi, vile vile katika upatikanaji. Ukiacha urembo na matumizi ya viwandani, “silver dust” hutumika kwenye cloud seeding (mabomu ya mvua).

Kwa wastani wa 10-15% ya Magema ya dhahabu ya kanda ya ziwa (Victorian Greenbelt) na 35-45% ya magema ya Lupa (Rukwa na Songwe) ni kiwango cha fedha kilichomo kwenye mwamba wa dhahabu! Ni sehemu chache duniani zenye magema yenye fedha kwa wingi kukaribia 100%.

Kuhusu mabomu ya mvua, ni kitu kipo! Mvuke angani ya mvua hutegemea chembe za vumbi kuunda matone ya mvua ila lazima halijoto ya angani iwe chini sana. Vumbi la Fedha hutumika kuharakisha mchakato huu wa kuunda matone na kusababisha mvua.

HELIUM: Hii ni moja ya gesi adimu lakini muhimu sana kwa maputo yanayoruka anga za juu kusoma hali ya hewa (weather baloons) na yale maputo kama ya Serengeti (Hot air baloon). Gesi hii pia ni sehemu ya mfumo wa Kuchomea chuma (arc welding) na katika mitambo ya MRI.

Gesi hii adimu imegundulika kwa wingi (mita za ujazo 1.53b) katika miamba iliyo chini ya Ziwa Rukwa, kwa viwango vitakavyofanya Tanzania kuwa mmoja wa wazalishaji wakubwa wa gesi hii yenye umuhimu kwa miongo mingi ijayo! Tujipange tu, michongo inakuja.

SHABA: Bila shaba tungepataje umeme? Simu? Redio? Runinga? Moja ya kiungo muhimu sana cha kusafirisha umeme katika hali mbalimbali, na ndio imesaidia kuleta mapinduzi makubwa ya teknolojia katika upande wa Umeme na Elektroniki.

Shaba hupatikana kwa wingi kwa majirani DRC na Zambia, lakini pia ukanda wa kati kuelekea ukanda wa ziwa Tanzania kuna uwepo wa Shaba nyingi iliyoshikamana na dhahabu na fedha.

URANIUM: Usiweke karibu na watoto/hata watu wazima. Urani ni madini yanayoongoza kwa kuwa mionzi mikali (radioactive) na ya uwezo mkubwa wa kuleta madhara ya kansa. Madini haya yana matumizi makubwa ya kijeshi katika silaza za nyuklia.

Ukanda wa kusini kuanzia maeneo ya ukingo wa Mbuga ya Selous na mkoa wa Ruvuma, kuna viashiria vya uwepo wa magema yaliyosheheni Urani ya kutosha kutingisha dunia. Ukiacha silaha, urani pia hutumika kuzalisha nishati kama umeme.

DHAHABU: Madini haya yenye hali ya ubati (metal) yenye mng’ao wa manjano (ipo pia dhahabu nyeupe) hujulikana sana kama urembo. Zamani dhahabu ilitumika kama chombo cha kubadilishana thamani, na ilitumika kununulia vitu, kulipa kodi kwa wafalme n.k.

Dhahabu ni muhimu sana katika teknolojia ya kompyuta. Dhahabu kutokana na uwezo wake kufinywa na kuwa uzi mwenbamba kupindukia bila kumomonyoka, imechangia sana katika kukua kwa teknolojia ya “microchips” inayotumika kwenye vifaa vya kisasa vya kieletroniki.

Pia DHAHABU kutokana na uwezo wake wa kustahimili joto la juu na kusharabu mionzi, hupakwa kwenye rockets ziendazo anga za juu kukinga joto kali litokanalo na msuguano na hewa, mionzi ya moja kwa moja ya jua na kukinga watu dhidi ya mionzi hiyo hatari ya anga za juu.

MATUMIZI REJEA: Je Wajua? Madini mengi yenye uhaba na thamani kama dhahabu, fedha, platinum na yale yenye umuhimu kama shaba na chuma huweza kurejelezwa matumizi (Recycling)? Hii itafanya pamoja na uhaba wake, kukuza uvumbuzi wa namna ya kurejeza matumizi ya madini haya adimu.

Na @PatNanyaro

Bitnami