Header Ad

zinazosomwa zaidi

Most Viewed

Majibu ya kisheria: Je! Ni kweli mwanaume akiishi na mwanamke kwa kipindi kirefu wanakuwa wameoana?

Na; Makendi Aloyce (Mwanasheria)

DHANA YA NDOA (PRESUMPTION OF MARRIAGE)

Ndugu msomaji, unaweza kuwa na maswali mengi juu ya wapenzi (mwanamke na mwanaume) wanaoishi pamoja kwa kipindi fulani au hata muda mrefu zaidi pasipo kuwa wanandoa. Moja ya swali ni msimamo wa sheria ya ndoa juu ya wapenzi hao. Je, sheria inatambua mahusiano hayo? Pia ni namna gani unaweza kuthibitisha mahakamani dhana hii? nafuu gani/zipi za kisheria zilizopo baina ya wapenzi hao baada ya kuachana (mahusiano yao kuvunjika)? Na maswali mengine kama hayo.

Muandishi makala hii amejaribu kwa kiasi kikubwa kufafanua dhana ya ndoa kwa mujibu wa sheria ya ndoa ya mwaka 1971.

Dhana ya ndoa yaani “presumption of marriage” kama jinsi maneno yalivyo, ni dhana inayojengwa kisheria kwa mwanaume na mwanamke wanaoishi pamoja pasipo kuwepo na ndoa rasmi. Sheria inaweka namna ambayo wapenzi hao watadhaniwa kua katika ndoa kutokana na namna au jinsi ya maisha wanayoishi, ni mahusiano ambayo hayakufuata taratibu rasmi zilizowekwa kisheria hivyo mikono ya mahakama hutumika kuamua msimamo wa kisheria juu ya mahusiano hayo.

Hivyo basi, kwa sheria zetu za Tanzania kuna dhana inayokanushika (rebuttable presumption) kuwa mwanaume na mwanamke wakiishi pamoja kwa miaka miwili au zaidi huchukuliwa kuwa ni mke na mume mbele ya jicho la sheria japokuwa hawakuwahi kufunga ndoa. Dhana hii imeelezwa katika kifungu cha 160 (1) na (2) cha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971.

Ili dhana hii ya uwepo wa ndoa iwepo ni lazima mambo yafuatayo yathibitishwe mbele ya mahakama;

Mosi, ni lazima ithibitike kwamba mwanamke na mwanamume wameishi pamoja kwa muda wa miaka miwili (2) au zaidi kwa mfululizo. Kama hawakuishi kwa muda wa miaka miwili au zaidi kama sharia inavyoelekeza, wawili hao watakua ni “mahawara” (concubine).

Pili, ni lazima ithibitike kuwa umma unaowazunguka unawachukulia na kuwapa heshima kama mke na mume (mfano ni namna gani majirani wanawachukulia wawili hawa, je, wanawaona kama wanandoa au marafiki wa kawaida tu yaani “boyfriend na girlfriend”?

Tatu, ni lazima ithibitishwe kuwa wawili hao walikuwa na uwezo wa kuwa mke na mume wakati walipoanza kuishi pamoja kama umri ulikubalika kisheria.

Mwisho, ni lazima pia ithibitishwe kuwa mmoja kati ya hao wawili au wote hakuna aliye na ndoa inayoendelea (subsisting marriage).

Kwanini dhana ya ndoa (why presumption of marriage)?

Imekua kawaida katika jamii zetu kwa mwanamke na mwanaume kuishi kama mume na mke pasipo kufunga ndoa rasmi kama sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inavyoelekeza. Kimsingi hakuna tatizo kwa wapenzi hao kuishi bila kufunga ndoa rasmi kama mahusiano yao ni ya furaha na amani, lakini mambo hugeuka machungu pale tu ambapo mahusiano hayo yanavunjika na kupelekea wapenzi hao kuomba msaada wa mahakama kuingilia kati. Msaada wa mahakama kisheria ni kutazama mahusiano hayo na kuangalia kama yanakidhi vipimo/vigezo vilivyowekwa kisheria ili kujua ni haki zipi wawili hao (pamoja na mtoto/watoto waliopatikana katika mahusiano hayo) wanazo katika mahusiano hayo.

Dhana ya ndoa inatambulika kisheria kwa sababu zifuatazo;

Kimsingi lengo kuu la dhana hii ni kuwalinda watoto wanaopatikana ndani ya mahusiano hayo pamoja na wahusika wenyewe katika ndoa dhanifu.

Wanawake/mwanamke; Lengo ni kuwalinda wanawake dhidi ya wanaume ‘wahuni” wenye lengo la kuwanyonya wanawake kwa kuwafanya kama wake zao na kuchuma mali kwa msaada ya wanawake hao lakini mwisho wa siku huwafukuza wakiwa mikono mitupu. Mwanamke ana haki ya kupata mgao wa mali walizochuma katika mahusiano hayo na mambo mengine kwa mujibu wa sheria ya ndoa ya mwaka 1971.

Watoto/mtoto; Kwa upande mwingine, inawezekana kabisa wawili hawa wakapata mtoto au watoto katika mahusiano yao. Watoto hawa hawana hatia yoyote na wana haki zao za msingi kisheria. Hivyo dhana hii inawapa watoto hawa haki ya kupata matunzo na malezi bora kama watoto wengine.

Hitimisho

Suala la msingi la kuzingatia ni kwamba, “dhana ya uwepo wa ndoa (presumption of marriage) haikusudii wala hailengi kuweka au kutengeneza njia mbadala za kufunga ndoa”. Jaji Mwalusanya alisisitiza hili katika kesi ya Zaina Ismail na Saidi Mkondo mwaka 1989. Na mwisho kabisa, pale tu dhana ya ndoa itakapokua imethibitika mbele ya mahakama, mahakama itaendelea kuchukua hatua nyingine za kawaida kabisa za kisheria kuvunja ndoa hio kama ndoa nyingine za kawaida zinavyofanyiwa kazi mbele ya mahakama.

Bitnami