Header Ad

zinazosomwa zaidi

Most Viewed

Mambo ya muhimu kufahamu kuelekea mchezo wa Simba na Yanga

Baada ya tambo za muda mrefu nje ya uwanja, hatimae siku ya kumaliza tambo hizo na kujua kama kuna mbabe au wote nguvu sawa imefika, ambapo shughuli nzima itakuwa pale kwa Mkapa.

Kama wasemavyo vijana wa kileo, habari ya mjini katika soka ni mchazo wa watani wa jadi, Simba SC na Yanga SC ambao ni mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Mashabiki wa kila upande wameonesha tambo kwamba timu yao ndiyo itakayoibuka na ushindi, lakini dakika 90 ndizo zitakazokuwa msema kweli, na kuonesha nani bingwa zaidi.

Licha ya tambo hizo, watu husema kuwa namba hazidanganyi, na kama hivyo ndivyo, basi Simba ina nafasi kubwa zaidi ya kushinda mchezo wa leo kuliko Yanga. Baada ya michezo 13 ya ligi, Simba imejikusanyia alama 34 ikiwa nafasi ya kwanza, ambapo Yanga baada ya michezo 11 ina alama 24 ikiwa nafasi 5. Hata kama Yanga ingekuwa imecheza mechi 13 na ikashinda hizo mbili ambazo bado haijacheza, bado ingekuwa nyumba ya Simba kwa alama 4.

Pia ushindi wa magoli baina ya timu hizi unaibeba sana Simba ambapo imekuwa ikipata ushindi kwa idadi kubwa zaidi ya magoli kuliko Yanga. Tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa ya Simba ni 34, wakati kwa Yanga tofauti ni magoli 6.

Mechi 5 za mwisho kwa kila timu msimu huu wa ligi, zote zimeshinda michezo minne na kwenda sare mchezo mmoja. Katika michezo hiyo Simba imefunga magoli 11 lakini haijafungwa kabisa, Yanga ikifunga magoli 7 na imefungwa magoli 3.

Katika mechi mbili za mwisho za watani wa jadi, Simba imeshinda mchezo mmoja kwa kuifunga Yanga 1-0, na mchezo mmoja ulimalizika suluhu.

Mpira hudunda, ndivyo wasemavyo mashabiki wa soka. Na kazi ya historia sio kutabiri kitakachotokea, bali kukuonesha ulipotoka.

Kulekea mchezo wa leo, hivi ndio vikosi vya mahasimu hao wawili:

Simba XI:

Aishi Manula, Gadiel Michael, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Sharaf Eldin Ali Shiboub, Jonas Mkude, Francis Kahata, Deo Kanda, Meddie Kagere Clatous Chama.

Yanga XI:

Farouk Shikhalo, Juma Abdul, Kevin Yondani, Ally Sonso, Adeyum Saleh, Mapinduzi Balama, Abdulaziz Makame, Deus Kaseke, Papi Tshishimbi, Ditram Nchimbi, Patrick Sibomana.

Katika historia, vipigo vikubwa zaidi kuwahi katika michezo ya Simba na Yanga ni kama ifuatavyo:

Mwaka 1968 Yanga iliifunga Simba magoli 5-0, kipigo hicho kikubwa zaidi kwa wakati huo kilidumu kwa miaka 9, kabla ya kisasi kulipwa ambapo mwaka mwaka 1977 Simba iliibaragaza Yanga kwa magoli 6-0. Huu ndio mchezo pekee wa watani wa jadi uliotoa ‘hat-trick’ iliyofungwa na Abdallah Kibadeni.

Bitnami