Header Ad

zinazosomwa zaidi

Most Viewed

Serikali yalifunga kanisa Moshi kutokana na mgogoro

Serikali ya Wilaya ya Moshi imelifunga kwa muda kanisa la Evangelist Assembles of God (E.A.G.T) Mawenzi lililopo Mtaa wa Vigae kutokana na mgogoro kati ya waumini na uongozi wa juu wa kanisa.

Chanzo cha mgogoro kinadaiwa kuwa ni uongozi wa juu wa kanisa hilo kumuondoa mchungaji mwanzilishi wa kanisa hilo katika mtaa huo, Frank Mushi na kumleta mchungaji mwingine pasi na ridhaa ya waumini.

Uongozi wa kanisa umesema sababu ya kumuondoa mchungaji huyo ni kutokuwa na elimu ya dini (theology), hivyo hajakidhi vigezo vya kutoa huduma kwa waumini.

Mmoja wa waumini wa kanisa hilo amesema kuwa uongozi wa kanisa ulikimbilia polisi, badala ya kumaliza mgogoro huo ndani ya kanisa kwa sababu wanataka kutumia nguvu kuleta mchungaji mpya na kumuondoa yule aliyekuwepo.

“Walikuja kutupa nje vyombo vya mchungaji na mchungaji akaondoka. Sisi tukabaki hapa kanisani tukiomba Mungu atausaidie, sasa sijui imefikaje huko kwa mkuu wa wilaya, na wakamshtaki mchungaji na makosa ya uongo. Sasa leo tukiwa tunasali, magari ya polisi yakaja, yakafunga,” amesema muumini huyo.

Amesema si kweli kwamba mchungaji huyo amekataa kwenda shule kusoma elimu ya dini kama ambavyo uongozi wa kanisa umedai, lakini alishindwa kwenda kwa sababu wakati wanamtaka aende alikuwa amevunjika mkono.

“Wanasema wamemfukuza kwa sababu amekataa kwenda kusoma Bible School (Shule ya Biblia), halafu na kipindi hicho alikuwa amevunjika mkono, na hadi sasa ni miaka 16 mkono haujaunga. angeenda vipi,” amehoji mmoja wa waumini.

Mbali na hilo, baadhi ya waumini wamedai kuwa sababu nyingine ya mchungaji wao kuondolewa ni nia ovu ya uongozi kutaka kuwageuza wao kama sehemu ya biashara kwani mchungaji aliyekuwepo alikuwa akitumia sadaka kujenga makanisa maeneo mbalimbali mkoani Kilimanjaro.

Wakati Frank Mushi anafukuzwa alikuwa tayari amepanda ngazi ya uongozi na kufikia kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo la Kilimanjaro.

Bitnami