Header Ad

zinazosomwa zaidi

Most Viewed

Mambo matano yakuepuka katika malezi ya watoto

Licha ya kuwa kila jamii ina mambo yake inayoyazingatia katika malezi, moja ya vitu ambazo jamii nyingi kwa ujumla zinakabiliana nazo ni changamoto ya malezi ya watoto.

Mbali na changamoto hiyo ipo mifumo kadhaa ambayo haibadiliki kwenye malezi karne hadi karne.

Changamoto hii huwa kubwa zaidi pale ambapo malezi hujumuisha watoto wa jinsia tofauti, na kwamba jinsia moja hupewa kipaumbele kikubwa zaidi kuliko jinsia nyingine.

Hapa chini ni baadhi ya masuala ya msingi ya kuzingatia kama wazazi au walezi katika malezi ya watoto wa kike na wa kiume;

Majukumu ya nyumbani
Watoto wote wanatakiwa kushiriki majukumu ya nyumbani bila kujali jinsia zao. Katika baadhi ya familia kumewekwa ratiba nzuri ambayo inaonesha nani atafanya nini wakati/siku gani.

Usimfanye mtoto wa kike kuwa mtumishi wa watoto wa kiume, kwamba watoto wa kiume wanapata muda wa kupumzika/kucheza huku wale wa kike wakifanya shughuli za nyumbani. Ni muhimu sana wakasaidiana kutimiza majukumu hayo.

Hili litawasaidia hasa watoto wa kiume inapofikia umri wa kujitegemea, kwani wataweza kutimiza majukumu ya msingi kama vile; kupika, kufua, kusafisha nyumba n.k. wenyewe, na pia itawawezesha kuwa waume na baba bora katika familia zao.

Heshima
Usimfunze mtoto wa kike kumuheshimu mtoto wa kiume kwa vile tu ni wa kiume. Baadhi ya wazazi huwaambia binti zao ‘kwanini unaongea na kaka yako namna hiyo, hujui yeye ni mwanaume?’ Hii si sahihi kwani inamjengea mtoto wa kiume kuwa wanapaswa kuheshimiwa na wanawake wakati wote na mwanamke hapaswi kupewa heshima, huku ikimjengea mtoto wakike nidhamu ya woga na kujiona kuwa hastahili kuheshimiwa.

Mjengee mwanao mazingira kujua kwamba heshima inatafutwa. Utaheshimiwa pale utakapoonesha unastahili heshima au utakapoheshimu watu wengine.

Udhaifu kwa mwanaume
Wajengee watoto wako wa kiume mazingira ya kuwaonesha kuwa mtoto wa kiume kushindwa, au kuumia kihisia ni sehemu ya maisha na kwamba kikubwa ni kuikabili hali hiyo na kuinuka tena.

Usimwambie mwanao “unaliaje kama wakike,” “wanaume hawaliagi,” kwa kusema hivi haumfanyi yeye kuwa imara, bali unamfanya awadharau watoto wa kike. Muoneshe kuwa kulia si jambo la kike bali ni la kibinadamu.

Usiwalinganishe kwa jinsia
Katika makuzi, usiwalinganishe au kupima mafanikio ya watoto kwa kutumia jinsia zao, bali yeyote atakayefanya vizuri mpongeze kwa kulingana na alichofanya.

Kuna wazazi ambao endapo mtoto wa kike atafanya vizuri kuliko wa kiume watawaambia wale wa kiume, “huoni aibu unashindwa na dada yako?” Kwa kufanya hivyo unamuaminisha kuwa mafanikio ni ya watoto wa kiume, na ni aibu mwanaume kushindwa na mwanamke.

Tenga muda
Vijana wa zama hizi husema kuwa mzazi asipompa mwanae “attention” atakwenda kuitafuta kwenye mitandao ya kijamii, na hilo linaweza kupelekea kufanya vitu vya ajabu ili apate hiyo “attention.”

Ni vyema mzazi ukatenga muda kwa watoto wote bila kijali jinsia zao. Baadhi ya wazazi hupendelea kutenga muda zaidi wa kukaa na kuzungumza na watoto wa kike, huku watoto wa kike wakishughulika na majukumu ya nyumbani.

wakati huo wakiwafunza binti zao kuwa wadada na wanawake bora huku wakisahau kufanya vivyo hivyo kwa wanao wa kiume.

Kikubwa cha kufahamu ni kuwa unapolea mtoto unalea mtu ambaye atakuja kuwa mke, au mume wa mtu, atakuwa na marafiki, atakuwa mzazi, atakuwa na majirani. Hivyo ni vyema kumlea kwa njia ambayo itamuwezesha kukaa vizuri ndani makundi hayo.

Bitnami