Baraza la Habari lawaanika walioambatana na Makonda kuvamia Clouds

872
0
Share:
Share this
CMTL Group

Baraza la Habari Tanzania (MCT) leo Jumatatu Agosti 14, 2017 limezindua ripoti mbili juu ya hali ya uhuru wa habari pamoja na tukio la uvamizi wa Kituo cha Clouds Media.

Katibu Mkuu wa MCT, Kajubi Mukajanga akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa ripoti hizo amesema tafiti hizo zinafanywa kama inavyoelekezwa na katiba ya baraza hilo, na kwamba wamekuwa wakizifanya tangu mwaka 2001 akitolea mfano wakati alipouawa David Mwangosi walituma timu ya watafiti, vilevile Serikali ilipozuia matangazo ya Bunge walifanya tafiti.

Akizichambua tafiti hizo, Mukajanga alisema tafiti hizo zimehusisha timu ya wataalamu wa sheria, vyombo vya usalama pamoja na
wanahabari.

Baraza hilo lilitoa jukumu la kuchunguza kilichotokea kituo cha Clouds Media Group 17 Machi, 2017 ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alienda studio usiku akiwa na askari.

MCT ilisema kuwa, kwa mujibu wa katiba ya habari kifungu cha tatu [E] ndicho kilichowasimamia katika uchunguzi wao ambapo timu hiyo ilikuwa na watu wanne.

Hadidu za rejea zilizotumika katika utafiti huo ni,  kwanza kuchunguza kilichotokea, kubaini askari walioambatana na Mkuu wa Mkoa, kutoa mapendekezo kutokana na uchunguzi, kuandika ripoti na kuwasilisha kwa wananchi.

Timu hiyo ilitembelea ofisi za Clouds Media Group na kuongea na baadhi ya wafanyakazi, ilifanya mahojiano na wafanyakazi wa TRA, na pia ilifanya mahojiano maafisa wa haki za bianadamu.

Aidha, baada ya kumaliza upande mmoja na kujaribu mkutafuta Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano, juhudi hizo hazikuzaa matunda yoyote.

Kufuatia uchunguzi huo, MCT ilibaini kuwa, tarehe 17 Machi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akiwa na askari alienda kwenye kituo cha Clouds usiku, lakini afisa wa ulinzi alisema kiongozi huyo huwa anaenda mara kwa mara na alishazoeleka.

Jambo jingine ni kuwa, hakuna ubaya kwa vyombo vya habari kushirikiana na wanasiasa, lakini urafiki uliojengwa kati ya Mkuu wa Mkoa na Clouds ndio uliopelekea akawa na ujasiri wa kuingia ofisi kwa namna ile.

Pia, Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilisema haina wajibu wa kumuadhibu mtu aliyekikosea kituo cha habari kwahiyo wanaona iwepo sheria itakayoruhusu TCRA kuweza kufanya hivyo.

Kuhusu walinzi walioambatana na RC Makonda, MCT ilisema kuwa ilithibitisha bila shaka kwamba baadhi ya Askari hao walikuwa kutoka Jeshi la Polisi na wengine kutoka Usalama wa Taifa (TISS). Hayo wamesema yalithibitishwa na Makonda mwenyewe alipokuwa akifanya mahojiano na Startv ambapo alisema kuwa wale walikuwa walinzi wake, na kwamba ulinzi wake uliimarishwa mara tu baada ya kuanza vita dhidi ya dawa za kulevya.

Mwenyekiti wa timu iliyochunguza uvamizi huo, Juma Thomas alisema kwamba, haijalishi sababu yoyote iliyomfanya kiongozi huyo kwenda Clouds kama alivyofanya, lakini alikiuka sheria za uhuru wa habari na uhuru wa wahariri.

Comments

error: Content is protected !!