Barua ya wazi kwa Watanzania wenzangu: Sheria na haki kamwe havitengani

544
0
Share:
Share this
CMTL Group

 

 

  Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kusema: “Sheria na Haki havitenganiki”. Katika hili alimaanisha kuwa, mfumo wetu wa sheria ufanye kazi kwa manufaa ya Watanzania na sio kikundi cha watu wachache wenye uwezo.

Jaji Mkuu mpya anatukumbusha tena kuhusu hili. Juma hili, Profesa Ibrahim Juma amewataka Watanzania kupaza sauti zao kuhusu rushwa katika mahakama.

Namna hii ya kujichunguza na kujitathmini mwenyewe unavutia. Wananchi wana haki ya kupata huduma za kimahakama, lakini haki itapatikana endapo tu mhimili wa mahakama itakuwa huru. Ni lazima mahakama iwe huru kutoka kwenye vitendo vya rushwa vinavyoiingilia na kusababisha haki kuto kutendeka.

Prof. Juma amewataka wananchi kumtaja mtumishi yeyote wa mahakama ambaye anakwamisha upatikanaji wa haki. Jaji Mkuu ana haki ya kusema hivyo, kwani kama mfumo wa kisheria wan nchi hauwatumikii wananchi wake, inatupasa wote kuurekebisha.

Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Hamis Juma akila kiapo cha Utumishi wa Umma mbele ya Rais Dkt Magufuli

Katika miaka ya hivi karibuni, watu wenye uwezo wa kifedha wametumia hongo na aina nyingine za rushwa kuukimbia mfumo wa haki. Kama jamii, ni lazima tusimame pamoja dhidi ya watu hawa pamoja na watumishi wa mahakama ambao wamekuwa wakipokea rushwa na kukwamisha haki kutendeka.

Chakushangaza Zaidi ni kwamba, watu hawa matajiri wameruhusiwa kuuteka mateka mfumo wa sheria wa Tanzania. Hivi majuzi nilikuwa nikisoma habari za watu kama Harbinder Seth, James Rugemalira na Yusuf Manji wakitumia utajiri wao kuchelewesha kesi dhidi yao.

Rais Dkt Magufuli amezitambua njama hizi na hivyo ameishauri mahakama kuwaondoa watumishi wanaopokea rushwa katika mfumo wa kisiasa.

      James Rugemalira na Harbinder Sethi Singh wakiwa mahakamani

Katika hutoba yake juma lililopita alisema: “Kuna sababu za msingi ambazo zinaweza kupelekea kuchelewesha haki, lakini baadhi ya kesi hazitakiwi kuwahirishwa kwa kipindi cha muda mrefu.” Rais ameishauri mahakama na taasisi nyingine za uchunguzi kubuni mbinu ambazo zitaweza kukabiliana na tatizo hilo.

Jaji Mkuu amewataka majaji wapya wanaokula viapo kutazamia katika kujifunza namna ya majaji bora.

“Mnapaswa kujifunza kutoka kwa makarani wa mahakama, wanasheria, majaji wenzenu, ambao mtakuwa mkifanya kazi pamoja.”

Rushwa sio tu kwamba ipo katika watu wenye nafasi za juu katika mfumo, rushwa inaweza kuwepo mahala popote pale penye uongozi.

Sio kwamba Watanzania wanataka tu haki katika mfumo wa kisheria, lakini hata wawekezaji wa kigeni huondoka kwa hofu pale wanapoona mambo hayaendi katika njia kama yalivyotakiwa. Wawekezaji hawa ni sehemu ya kampuni ambazo huleta ajira na ubunifu nchini. Hivyo ni lazima kuwepo na namna ya kuzilinda ziendelee kusalia, kama zinafuata sheria na taratibu za nchi.

Baadhi ya wawekezaji hawa, wamekumbwa na madhalimu makubwa sana katika mfumo wetu wa kisiasa. Kucheleweshwa kwa kesi, watumishi wala rushwa, na matatizo ya kiuongozi ni miongoni mwa matatizo ambayo wanakumbana nayo.

 

Yusuf Manji akiwa mahakamani. Manji amefutiwa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.

Februari Mosi mwaka huu, Rais Dkt Magufuli alimteua Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dr. Adelardus Kilangi. Kilangi atakuwa nguzo nyingine muhimu kati vita dhidi ya rushwa. Licha ya kuwa sura hizi mpya zinatoa matumaini kwa Tanzania ijayo, lakini matumaini ya kweli yapo mikononi mwa Watanzania. Ni lazima tuwawajibishe majaji, watumishi wa mahakama na maafisa wengine kuhakikishe kuwa rushwa inatokomezwa.

Imefika wakati sasa tuseme imetosha kwa watu wenye utajiri kuugeuza mfumo wetu wa kisheria kama kitu kisicho cha maana. Kwa kufanya hivyo, mfumo wetu wa haki utaweza kuwa kama vile Baba wa Taifa alivyokuwa akitazamia uwe.

 

Mpaka wakati mwingine,

 

Ndugu yenu,

 

Wanzagi N. Talewa

Butiama, Mara

——————————————————————————————————————————————————————————————————————————

***Maoni ya waandishi wa makala sio msimamo wa Swahili Times. Kumbuka, nawe pia unaweza kututumia makala, kero au uchambuzi wako kwa: habari@swahilitimes.com****

Comments

error: Content is protected !!