Huu hapa wasifu wa Mkurugenzi Mtendaji Mteule wa Vodacom Tanzania Sylvia Mulinge

1299
0
Share:
Share this
  • 2.2K
    Shares

Imeandikwa na Ally Shekifu (University of Dar es Salaam Business School)

Sylvia Mulinge ni nani?

Sylvia Wairimu Mulinge, Mkuu wa Idara ya Wateja (Consumer Business Unit) katika kampuni ya mawasiliano ya Safaricom nchini Kenya

Sylvia Wairimu Mulinge (Sylvia Wairimu), ni mwanamke mfanyabiashara na kinara wa uongozi wa makampuni wa katika eneo la Afrika Mashariki. Kwa sasa, Mulinge anahudumu kama Mkuu wa Idara ya Wateja (Consumer Business Unit) kwenye kampuni ya mawasiliano ya Safaricom nchini Kenya. Safaricom ndiyo kampuni kubwa zaidi ya mawasiliano Afrika Mashariki kwa kigezo cha mapato, ambapo mwaka 2017 ilikuwa na mapato ya kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 968,880.

Mulinge ni Mhitimu wa Shahada ya Kwanza ya Heshima katika Sayansi ya Vyakula na Teknolojia kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na ni mwanachama wa Kundi la Wataalamu wa Masoko nchini Kenya. Jarida la Business Daily ambalo ni moja ya machapisho yanayoheshimika sana Afrika Mashariki limemuorodhesha Mulinge kama mmoja wa wanawake 40 wenye umri chini ya miaka 40 ambao wana ushawishi mkubwa zaidi.

Safari kuelekea nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji Vodacom Tanzania

Sylvia amehudumu kwa zaidi ya muongo mmoja katika eneo la masoko, nusu ya muda huo ikiwa ni katika makampuni ya mawasiliano na ni mtu mwenye uwezo mkubwa katika nyanja ya huduma kwa wateja, ubunifu katika teknolojia na kukuza biashara.

Mulinge alijiunga na kampuni ya Safaricom nchini Kenya mwezi Februari mwaka 2006 akitokea kampuni nyingine nguli ya Uniliver. Baada ya kuingia Safaricom, juhudi zake katika utendaji zilimpandisha nafasi haraka kutoka Msimamizi wa Kitengo cha Malipo Kabla ( Prepay Product Manager) hadi Mkuu wa Idara ya Rejareja (Head of Retail) ambako aliongoza nguvu kazi ya kampuni hiyo katika mauzo ya rejareja ya uuzaji simu kutoka shilingi za Kitanzania bilioni 6 hadi shilingi bilioni 34 katika kipindi cha miaka miwili tu.

Ni utendaji wake huu wa kiwango cha juu ambao ulisababisha kuteuliwa kwake kuwa Meneja wa Jumla wa Kitengo cha Biashara cha Safaricom mwaka 2011, akiwa una umri mdogo wa miaka 34. Katika jukumu hilo jipya Sylvia anakumbukwa kwa kuibadili Safaricom kibiashara na kuingia katika utoaji huduma za mtandao wa intaneti ikilenga makampuni makubwa, kuwezesha kukua kwa soko la ubunifu kwa biashara ndogondogo na za kati na kukuza mauzo ya kitengo hicho hadi kufikia shilingi za Kitanzania bilioni 3 kwa mwezi, sawa na shilingi milioni 100 kila siku.

Mwezi Machi mwaka 2015 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara Safaricom. Kwa miaka mitatu katika nafasi hiyo amekuza mafanikio ya kibiashara kwa mbinu mbalimbali

kama kubuni huduma mahalia, na huduma za makundi ambazo zimeboresha maisha ya mamilioni ya wateja.

Mpaka hapa utaona kuwa mwanamke huyu, zao la Jumuiya ya Afrika Mashariki amekuwa nguzo muhimu ya ukuaji wa Safaricom katika huduma yake kwa wateja zaidi ya milioni 29.5 na mapato zaidi ya trilioni 4 za Kitanzania huku kitengo anachoongoza Mulinge kikiwa kinachangia zaidi ya asilimia 25 ya mapato hayo.

Nguli mwingine wa uongozi katika makampuni ya mawasiliano Afrika ya Mashariki, Bob Collymore (pia Mkurugenzi Mtendaji wa Safaricom) anasema, “Kwa miaka yake 17 katika kazi hii na miaka 10 kati ya hiyo akiwa Safaricom, Sylivia amejijengea heshima kama moja ya viongozi mahiri katika kuendesha biashara na mtu ambaye ameshika usukani wa kuiweka kampuni imara katika nyakati ngumu”.

Jukumu lake jipya

Kama Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Vodacom Tanzania, Sylvia atakuwa anaripoti kwa Diego Gutierrez, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Biashara cha Vodacom Group. Uteuzi wake ni ishara tosha ya weledi, umakini na uzingatiaji wa jinsia ambao Vodacom imeonyesha katika kufanya biashara. Uteuzi huu unaonyesha nia ya Vodacom katika kupigia chapuo maendeleo ya wanawake na uwakilishi wao katika uongozi na utawala. Sylvia ni mwanamke wa pili kuteuliwa na Vodafone duniani kuwa Mkurugenzi Mtendaji. Bi Murielle Lorilloux, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Vodafone Romania alikuwa wa kwanza kushika nafasi hiyo.

 

Comments

error: Content is protected !!