Jeshi la Polisi laamua ‘kumpuuza’ Dkt. Louis Shika

650
0
Share:
Share this

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema hawataendelea na kesi dhidi ya Dk Louis Shika kwa kuwa nyumba tatu za mfanyabiashara maarufu Said Lugumi alizoahidi kuzinunua zote zipo.

Novemba 9 mwaka huu Kampuni ya Udalali ya Yono kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliendesha mnada wa nyumba mbili za Lugumi zilizoko Mbweni JKT na moja Upanga jijini Dar es Salaam ambazo zote Dk Shika alifikia bei ya kuzinunua kwa Sh3.2 bilioni.

Mambosasa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari amesema kesi yake haina mashiko hivyo hawataendelea nayo kwa kuwa nyumba hizo zipo na hajatia hasara.

Amesema Dk Shika alikuwa akitamba kuwa ana fedha kumbe uwezo wake ni mdogo na kusababisha  kushindwa kulipa asilimia 25 kwa kila nyumba hizo.

‘‘Dk Shika ni wa kumuonea huruma hana kitu tulisema tunamchunguza na tutampeleka mahakamani lakini tumeona kesi yake haina mashiko ndiyo maana hatuendelei nayo,” amesema Mambosasa.

Jeshi la Polisi lilimshikilia na kumwachia kwa dhamana Dk Shika ambaye alikuwa akituhumiwa kwa kuharibu mnada baada ya kushindwa kulipa asilimia 25 ya fedha hizo ambapo nyumba za Mbweni JKT alifika bei kwa Tsh 900 milioni na nyingine Sh1.1 bilioni, huku ya Upanga alifika bei ya Sh1.2 bilioni

 

Comments

error: Content is protected !!