Kiongozi wa CCM apinga hoja ya kuongeza muda wa Rais madarakani

749
0
Share:
Share this
CMTL Group

Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee Pius Msekwa amesema kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) hakitokubali kuongeza muda wa Rais kuwa miaka 7 kutoka miaka mitano ya sasa.

Mzee Msekwa aliyasema hayo jana alipokuwa akifanya mahojiano na Kituo cha Azam baada ya mjadala mzito kuibuka kuhusu nia ya Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM) kuwasilisha bungeni hoja binafsi akitaka muda wa Rais uongezwe hadi miaka 7 kama ilivyo kwa taifa la Rwanda.

Akitoa maoni yake, Mzee Msekwa alisema kuwa kipindi cha nyuma waliwahi kuwa na mjadala kama huo lakini Mwalimu Nyerere alikataa na ndipo walipitisha miaka 5 ambapo mtu ataweza kugombea kwa awamu mbili ambayo itafanya miaka 10.

“… Mwalimu Nyerere akashauri tufanye miaka 5 mara mbili, miaka 10 inatosha. Mkipata kiongozi mbaya, miaka 15 ni mingi sana, msisahau hilo,” alisema Mzee Msekwa.

Msekwa alieleza kuwa, mbunge huyo anayeleta hoja ya kuwa muda wa Rais madarakani uongezwe, ajue tu kwamba hilo si wazo jipya na kwamba huko nyuma walishawahi kulifikiria lakini likakataliwa.

“… mimi nina imani CCM itaendelea kulikataa hilo, tutabaki kwenye miaka mitano, mara mbili, basi.”

Alisema kwamba, haamini kama chama kipo katika nafasi ya kuweza kufikiria hoja ambayo kiliwahi kuikataa huko nyuma.

Kwa upande wake mtoa hoja, Juma Nkamia amesema kuwa hoja yake bado haijapelekwa kwa umma na kwamba hakuna mahali alipomtaja Rais badala yake anazungumzia ukomo wa Bunge.

Nkamia amefafanua kwamba, gharama zinazotumika kwenye chaguzi ni kubwa sana na hivyo miaka mitano inakuwa ni michache na kupelekea serikali kutumia gharama sana, hivyo ikiwa miaka saba, itaongeza unafuu.

Lakini mbali na hilo, Nkamia amesema kwamba, anapendekeza uchaguzi wa serikali za mitaa ufanyike pamoja na uchaguzi wa serikali kuu ili kupunguza gharama. Ina maana kwamba, uchaguzi ukifanyika pamoja, mpigakura atapiga kura kumchagua Mwenyekiti wa Kijiji au Mtaa, Diwani, Mbunge na Rais.

Mbali na Nkamia, Mbunge wa Tarime Vijijini (CHADEMA), John Heche alisema anakusudia kuwasilisha bungeni hoja binafsi ili kupunguza muda wa viongozi kukaa madarakani kutoka miaka mitano iwe miaka minne kama Marekani.

“”Nakusudia kuwasilisha bungeni hoja binafsi kupunguza muda wa kukaa madarakani kwa Rais, wabunge na madiwani kutoka miaka 5 mpaka 4 tuwe kama Marekani ili kutoa nafasi kwa wananchi kuwa na maamuzi zaidi kuhusu uendeshaji wa nchi yao.” 

Comments

error: Content is protected !!