Maagizo ya Rais Magufuli baada ya kupokea ripoti ya uchunguzi wa Tanzanite na Almasi

1066
0
Share:
Share this
CMTL Group

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 07 Septemba, 2017 amepokea taarifa za kamati maalum mbili za Wabunge zilizoundwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai kuchunguza biashara ya madini ya Tanzanite na Almasi hapa nchini.

Taarifa hizo zimekabidhiwa kwa Mhe. Rais Magufuli na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa Ikulu Jijini Dar es Salaam na tukio hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai, Mawaziri, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa Dini na viongozi wa vyama vya siasa.

Katika salamu zao Mwenyekiti wa Kamati ya Wabunge iliyochunguza madini ya Tanzanite Mhe. Doto Mashaka Biteko na Mwenyekiti wa Kamati iliyochunguza madini ya Almasi Mhe. Mussa Azzan Zungu wameleeza namna nchi inavyopoteza fedha nyingi kutokana na udanganyifu na wizi katika biashara ya madini hayo na wametoa mapendekezo kadhaa yakiwemo kurekebishwa kwa dosari za kimfumo, usimamizi na kuchukua hatua dhidi ya waliohusika kusababisha Taifa kupoteza fedha hizo.

Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai ameungana na Wabunge wa kamati alizoziunda kumpongeza Mhe. Rais Magufuli kwa dhamira yake ya kuchunguza biashara za madini hapa nchini na ametaka wananchi wamuunge mkono kama ambavyo Wabunge wanafanya.

Kabla ya kukabidhi taarifa hizo kwa Mhe. Rais, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amezishukuru kamati maalum zilizofanya uchunguzi huo na ametoa wito kwa Watanzania kuwa wazalendo na kujenga umoja na mshikamano katika kutetea rasilimali za Taifa, ili zinufaishe kizazi cha sasa na kijacho.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa taarifa hizo Mhe. Rais Magufuli amempongeza Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai kwa kuunda kamati maalum zilizofanya uchunguzi huo, amewapongeza Wabunge wa kamati hizo kwa kazi waliyoifanya na ameahidi kufanyia kazi mapendekezo waliyoyatoa.

Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali imedhamiria kuchukua hatua za kutetea rasilimali za Taifa kwa maslahi mapana ya wananchi na amesema inachukua hatua hizi ikiwa ina taarifa zote za udanyanyifu na wizi uliofanyika katika migodi ya madini na maeneo mengine.

Mhe. Dkt. Magufuli amekabidhi taarifa hizo kwa viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na ameagiza uchunguzi ufanyike ili wote waliohusika kusababisha upotevu mkubwa wa fedha za umma wachukuliwe hatua za kisheria haraka na pia amewaagiza viongozi hao kuweka ulinzi katika maeneo yenye rasilimali za Taifa ikiwemo migodi ya Tanzanite na Almasi.

Mhe. Rais Magufuli amewataka viongozi na watendaji waliotajwa katika ripoti hizo popote walipo wakiwemo wateule wa Rais wachukue hatua za kiuwajibikaji wakati uchunguzi unaendelea kufanywa.

“Wale ambao wametajwatajwa katika taarifa hii ambao ni wateule wangu, labda ni Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Katibu Tawala wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi, inawezekana walifanya kazi mahali pengine na sasa wapo mahali pengine lakini wametajwa kwenye taarifa hii, ili vyombo vya ulinzi na usalama vifanye kazi vizuri, ni matumaini yangu watalizingatia hili, ni matumaini yangu watakaa pembeni” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kuwakutanisha wataalamu na wajumbe wa kamati hizo maalum za Wabunge ili wajadiliane na kuanzisha mchakato wa kurekebisha sheria na mifumo ambayo inatoa mianya ya udanyangifu na wizi wa rasilimali za Taifa.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

07 Septemba, 2017

Comments

error: Content is protected !!