Mahakama yakubali ombi la aliyetaka apewe adhabu kali kama fundisho kwa wengine

682
0
Share:
Share this
CMTL Group

MAHAKAMA ya Wilaya ya Mlele mkoani Katavi imemhukumu kifungo cha miaka 40 jela mfungwa Juma Masasila (38) baada ya kumuona na hatia ya makosa matatu ya kumiliki nyara za serikali kinyume cha sheria.

Katika utetezi wake, mshtakiwa aliwashangaza watu baada ya kuiomba Mahakama impatie adhabu kali kutokana na kosa hilo ili iwe fundisho kwa wengine.

Masasila, ambaye alikuwa mkazi wa kijiji cha Songambele wilayani Mlele alikuwa akihudhuria mahakamani akitokea gerezani anakotumikia kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya kumiliki silaha aina ya gobore na kufanyia ujangili katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi.

Hukumu ya kifungo cha miaka 40 jela ilitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, Teotimus Swai baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa Jamhuri.

Awali, Mwendesha Mashtaka wakili wa serikali, Missy Malisimbo alisema mahakamani hapo kwamba mshtakiwa alikamatwa Januari 19 mwaka huu nyakati za saa 12:51 nyumbani kwake; akiwa na nyara za serikali ambazo ni pembe mbili na miguu minne ya isha, ngozi mbili za nungunungu na pembe tisa za ngiri.

Alisema baada ya mshtakiwa kufikishwa mahakamani alikana kukutwa na nyara hizo ndipo upande wa mashtaka ulipopeleka mashahidi saba ambao waliithibishia Mahakama kwamba Masasila alitenda kosa hilo.

Kabla ya kutoa hukumu hiyo, wakili wa serikali Malisimbo aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Swai alisema pasi na shaka Mahakama imemkuta na hatia mtuhumiwa hivyo anahukumiwa kwenda jela miaka 40.

Alisema kosa la kwanza la kukutwa na pembe mbili na miguu minne ya isha adhabu yake ni kifungo cha miaka 20 jela, huku kosa la pili kukutwa na ngozi mbili za nungunungu alitakiwa kulipa faini ya Sh. milioni 2 au kifungo cha jela miaka 10.

Alieleza kwamba kosa la kukutwa na pembe tisa za ngiri alipaswa kulipa faini ya Sh. 900,000 au kifungo cha miaka 10.

Mshtakiwa hakuwa na uwezo wa kulipa faini hivyo na amekwenda jela kutumikia adhabu ya miaka 40 juu ya mitano ya awali.

HT @ NIPASHE

Comments

error: Content is protected !!