Majina ya wafanyabiashara ya dawa za kulevya sasa wazi

631
0
Share:
Share this
  • 1.4K
    Shares

Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema inayo majina ya watu wanaojihusisha na biashara ya mihadarati mikoani na kwamba inaanza operesheni maalum kwa ajili ya kuwakamata.

Kamishna wa Intelijensia wa DCEA, Fredrick Kibuta, alieleza kuwa tayari wana majina ya watu wanaojihusisha na biashara hiyo mikoani hivyo wanakwenda kuwasaka, ili wachukuliwe hatua.

“Hatutaki kutaja ni lini, lakini wanaofanya biashara ya dawa za kulevya mikoani hawatajua saa wala muda,” alisema Kamishna Kibuta na kueleza zaidi, ” Tutawanasa”.

“Mamlaka ina mipango mingi na ina watu ambao tunawafuatilia na kwa sasa tunahamia mikoani kwa ajili ya operesheni (maana) lengo letu ni kutokomeza hii biashara haramu.”

‘Wazungu’ wa ‘unga’ 849 wakubwa na wadogo, wengi wao kutoka Dar es Salaam, walikamatwa katika kipindi cha kuanzia Februari hadi Desemba 31, mwaka jana.

Aidha, kesi 475 zilifunguliwa katika mahakama mbalimbali katika kipindi hicho na zinaendelea kusikilizwa.

Kamshina Kibuta alisema serikali inaendelea kuunganisha nguvu kwa kushirikiana na wananchi katika kuwafahamu wanaojihusisha na biashara hiyo pamoja na mbinu wanazozitumia.

Kamishna Kibuta pia alisema kumalizika kwa tatizo la dawa za kulevya ni jambo linalowezekana na kwamba wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuziondoa sokoni kwa kuwakamata wahusika wa biashara hiyo.

Kamishna Kibuta alisema kuwa tatizo la dawa za kulevya ni la dunia sio Tanzania peke yake na kwamba suala hilo ni jambo la uhalifu unaovuka mipaka.

“Wanaofanya biashara Tanzania wana mahusiano ya biashara na wa kimataifa na kila nchi ina mazingira yake ambayo yanaweza kuwapa faida au ugumu wafanyabiashara wa dawa za kulevya kushindwa kufanya biashara hiyo,” alisema.

Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja wa uhai wa DCEA wameendelea kufanya juhudi mbalimbali pamoja na kuwaelewa wafanyabiashara wa dawa za kulevya na kuona kipi cha kufanya ili kutatua tatizo hilo.

“Sisi kama mamlaka tunaona Tanzania bila dawa za kulevya inawezekana.” Alisema wanachokiomba wananchi kuendelea kuunga mkono mamlaka na kushirikiana katika mapambano ya dawa za kulevya.

Aidha, Kamshina Kibuta alisema mamlaka hiyo imekuwa ikijitahidi kuja na mbinu mpya kila wakati katika kupambana na tatizo hilo kwa kuwa wanaojihusisha na biashara hiyo huwa wanabadili mbinu zao pia.

“Hawa wafanyabiashara tumejitahidi kupambana nao; kila wanapokuja na mbinu zao sisi tunajitahidi kuwazidi, yaani tunakuwa mbele kuwazidi,” alisema Kamishna Kibuta.

“Katika mapambano haya hawawezi kutuzidi. Tuna mikakati mikali ambayo hawawezi kutuzidi. “Dawa ambazo zipo mtaani ni chache na tutakwenda kuzimaliza na wale wafanyabiashara wakubwa wa biashara hiyo tumeshawakamata na wapo gerezani ndio maana nasema mapambano yetu yanaenda vizuri.”

Adhabu kwa washtakiwa katika kesi hizo ni kifungo cha miaka 30 jela bila faini kwa mfanyabiashara aliyekutwa na kiwango kisichozidi gramu 20 na maisha jela kwa aliyezidi gramu hizo, kwa mujibu wa marekebisho ya Sheria Namba 5 ya mwaka 2015 (Sheria ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya) yaliyofanyika Novemba mwaka jana.

Februari 11, mwaka jana, Rais John Magufuli alimteua Rogers Siyanga kuwa Kamishna Mkuu wa DCEA ambayo ilikaa bila kiongozi tangu Sheria ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya ilipotungwa mwaka 2015 na kuizindua mamkala hiyo.

Comments

error: Content is protected !!