Mambo ambayo Lulu anaruhusiwa na asiyoruhusiwa kufanya akitumikia kifungo cha nje

263
0
Share:
Share this
CMTL Group

Kwa mujibu wa kifungu na 3(2) (a) cha Sheria ya Huduma kwa Jamii ya mwaka 2002 kifungo cha nje ni utaratibu ambao unampa fursa mfungwa kutumikia kifungo chake nje ya gereza kwa kufanya shughuli/kazi zisizo na malipo kwa manufaa ya jamii.

Utaratibu huu hutolewa kwa wafungwa ambao vifungo vyao havizidi miaka mitatu bila kujali wana faini au hawana.

Baada ya Mwigizaji Elizabeth Michael maarufu Lulu kupewa kifungo cha nje jana, watu wengi wamekuwa wakijiuliza imekuwaje akapewa kifungo hicho, lakini wapo pia waliokuwa wakijiuliza, baada ya kupewa kifungo cha nje, ni mambo gani mengi anaruhusiwa kufanya au harusiwi kufanya?

Mfungwa anapopewa kifungo cha nje, hakuna masharti ya jumla yanayofanana kwa wafungwa wote kwamba watakapokuwa nje ya gereza watatakiwa kufanya hiki na hawatakiwa kufanya kile.

Kifungu cha 4 cha Sheria za Huduma za Jamii kinaipa mahakama nguvu ya kuweka masharti kwa mfungwa atakayekuwa anatumikia kifungo cha nje, ambapo atatakiwa kuhakikisha hakiuki masharti hayo.

Miongoni mwa masharti ambayo mahakama humuwekea mfungwa wa aina hiyo ni pamoja na kwenda kuripoti kwa msimamizi wa huduma za jamii katika eneo husika, lakini pia kuhakikisha kuwa shughuli aliyopangiwa kuifanya anapotumikia kifungo chake nje ya jamii anaifanya kikamilifu.

Pia mahakama huweka sharti kuwa, endapo mfungwa huyo atabadilisha eneo la makazi, lazima atoe taarifa kwa msimamizi wake wa huduma za jamii.

Masuala mengine kama kusafiri (kutoka nje ya mkoa), kuajiriwa, kuendelea na masomo, au kufanya jambo jingine lolote kunategemeana na masharti yaliyowekwa na mahakama. Endapo mahakama haitakuwa imemzuia mfungwa kusafiri, basi atakuwa huru kusafiri, lakini akiwekewa zuio, hatopaswa kusafiri hadi hapo kifungo chake kitakapomalizika.

Pia mahakama huweka sharti kuwa, ndani ya muda anaotumikia kifungo cha nje, hatakiwi kutenda kosa jingine, na endapo atatenda josa jingine, atarejeshwa gerezani kuendelea na kifungo chake.

Shughuli ambazo mfungwa wa nje anaweza kupangiwa kufanya ni pamoja na kufanya usafi katika maeneo mbalimbali mfano shule, hospitali, kwenye fukwe au kushiriki katika shughuli nyingine za kijamii mfano shughuli za mazingira, ujenzi.

Comments

error: Content is protected !!