Mambo yakufahamu kuhusu Maktaba mpya ya UDSM inayozinduliwa leo

410
0
Share:
Share this
  • 681
    Shares

Rais Dkt John Pombe Magufuli leo Novemba 27, 2018 anakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maktaba kubwa na ya kisasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), na sherehe hiyo inafanyika katika eneo la maktaba hiyo mpya, Kampasi ya Mwalimu Julius Nyerere, Mlimani.

Wakati Rais akizindua maktaba hiyo, ni vyema tukafahamu mambo mbalimbali ya msingi kuhusu maktaba hiyo ya aina yake.

Jiwe la msingi la maktaba hiyo liliwekwa na Rais Dkt Magufuli  tarehe 02 Juni, 2016 ambapo kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, maktaba hiyo ndio maktaba bora kuliko zote barani Afrika.

Maktaba hiyo imejengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kupitia Kampuni ya Ujenzi ya Jiangsu Jiangdu kutoka China. Serikali ya china ilitoa msaada wa dola za Marekani zaidi ya milioni 41 kwa ajili ya ujenzi huo.

Mradi umejumuisha majengo mawili, moja la Maktaba yenyewe na lingine la Taasisi ya Confucius ambayo imekuwa ikifundisha lugha na tamaduni za Kichina kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Watanzania wengine. Majengo yote mawili yanachukua eneo la mita za mraba takribani 20,000.

Ndani ya Jengo la Maktaba kuna maeneo mbalimbali, yakiwa ni pamoja na sehemu za kuwekea makasha ya vitabu, maeneo ya kusomea vitabu na vitabu-pepe, ofisi za wafanyakazi na ukumbi wa kisasa wa mihadhara. Maktaba hii ina uwezo wa kukalisha wasomaji wapatao 2,100 kwa wakati mmoja na makasha yenye uwezo wa kuweka vitabu 800,000.

Pia Maktaba hii mpya ina ukumbi wa mikutano wenye uwezo wa kukaa watu 600. Maktaba mpya itasaidia sana kupunguza uhaba wa eneo na vifaa vya kusomea wanafunzi kwani ina vifaa na kompyuta za kisasa zenye programu za kuweza kupata machapisho mbalimbali duniani.

Comments

error: Content is protected !!