Mamlaka za Tanzania zilimshinikiza Balozi wetu- Umoja wa Ulaya

530
0
Share:
Share this
  • 528
    Shares

Umoja wa Ulaya (EU) umesema kuwa mamlaka nchini Tanzania zilikuwa zikimshinikiza Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Balozi Roeland van de Geer, na hivyo kupelekea kuondolewa nchini, na kuitwa kwa ajili ya mazungumzo.

Hayo yamesemwa na umoja huo leo katika taarifa iliyotolewa ikielezea masikitiko yao kuhusu hali ya kisiasa nchini Tanzania, ambayo inapelekea kuminywa kwa haki za binadamu, uhuru wa vyombo vya habari, vyama vya siasa pamoja na mazingira ya kufanya kazi kwa asasi za kiraia.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa na Mwakilishi wa EU, Federica Mogherini kwa niaba ya EU kuhusi uhusiano wa EU na Tanzania, umoja huo umesema kuwa, matukio yanayoendelea nchini Tanzania, hayaendani na uhusiano wa muda mrefu uliojengwa baina ya pande hizo mbili.

EU haikubainisha wazi katika taarifa zake kuwa mwakilishi huyo alikuwa akishinikizwa kufanya nini, lakini imezitaka mamlaka za Tanzania kutoweka mashinikizo katika shughuli za kidiplomasia.

Kutokana na mazingira hayo, EU pamoja na wanachama wake wameridhia kufanya mapitio ya kina ya kisera kuhusu Tanzania, na kuwa watafanya mazungumzo ya kisiasa na serikali ya Tanzania mara mapitio ya uhusiano baina ya pande hizi mbili yatakapokamilika, kwa lengo la kurejesha ushirikiano wenye tija kwa wote.

Wakati hayo yakiendela, umoja huo umesema utaendelea kushirikiana na wadau wengine katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kitamaduni, ikiwa ni pamoja na asasi za kirai.

Umoja wa Ulaya pamoja na wanachama wake umeeleza kuwa upo tayari kuendeleza ushirikiano na Tanzania ambao utakuwa ni imara na wakuheshimu misingi ya demokrasia.

Comments

error: Content is protected !!