Mawaziri wanne wamekiuka sheria kumjibu Mkaguzi Mkuu (CAG)- Zitto Kabwe

419
0
Share:
Share this
  • 307
    Shares
CMTL Group

Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kuwa Mawaziri wanaojibu hoja zilizoibuliwa na Madhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wanakiuka sheria, na kulitaka Bunge kuwachukulia hatua viongozi hao wa serikali.

Zitto Kabwe ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari alipokuwa akichambua ripoti ya CAG na kuonesha mambo mbalimbali kwa taifa ambayo yanatakiwa kushughulikiwa kwa haraka.

Katika taarifa hiyo walioitoa kwa waandishi wa habari, kiongozi huyo ameainisha maeneo manane yaliyoibuliwa na CAG ambayo ni hatari kwa taifa.

Miongoni mwa mambo hayo hatari aliyoyazungumzia ni suala la mawaziri kujibu hoja za CAG mbele ya waandishi wa habari.

Hadi sasa, Mawaziri ambao tayari wamejibu hoja za CAG ni wanne ambao ni, Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt Mwakyembe, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Philip Mpango, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemani Jafo

“Kisheria mikutano hii ya Mawaziri na wanahabari inayoendelea ni kinyume na Sheria ya Ukaguzi ya Umma, kifungu cha 38(1) na (2), ambacho kinaelekeza waziwazi kuwa Maafisa Masuuli ndio wanapaswa kujibu hoja za ukaguzi zilizoibuliwa na CAG.”

Amesema, hata hivyo, Maafisa Masuuli hawatakiwi kutoa maelezo au kujibu hoja zilizoibuliwa na CAG mbele ya waandishi wa habari, badala yake wanatakiwa kupelekea taarifa zao katika Kamati za Kudumu za Bunge (PAC na LAAC).

“Majibu husika hupaswa kuletwa mbele ya Kamati za Bunge za PAC na LAAC. Kwa utaratibu wa kawaida wa kiwizara, Maafisa Masuuli ni Makatibu Wakuu wa Wizara na si Mawaziri,” alisema Zitto.

Kufuatia uvunjifu huo wa sheria, Zitto amewaomba Wenyeviti wa Kamati za Bunge za PAC na LAAC kufikisha suala Mawaziri kuzungumza kwenye vyombo vya habari kujibu ripoti ya CAG kwa Spika wa Bunge, ili Spika amjulishe Waziri Mkuu juu uvunjifu huu wa sheria unaofanywa na Mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano, wakiwemo Mawaziri wazoefu wa taratibu za kibunge kama Waziri William Lukuvi na Waziri Harrison Mwakyembe.

Aidha, Zitto amesema kwamba, kinachofanywa na Mawziri hao ni kuwahadaa wananchi ili kusahau hoja za msingi zilizoibuliwa na CAG, na hivyo kuwataka waache mara moja.

Comments

error: Content is protected !!