Mbunge wa CCM akamatwa kwa kusababisha kifo cha mwanafunzi

531
0
Share:
Share this
CMTL Group

Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida linamshikilia Mbunge wa Jimbo la Manyoni Daniel Mtuka (CCM) kwa tuhuma ya kumgonga kwa gari na kumsababishia kifo mwanafunzi wa darasa la kwanza wa Shule ya Msingi Sukamahela, Salome Paschal (10).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, ACP Debora Magilingimba, alisema tukio hilo lilitokea Agosti 10 katika Kijiji cha Sukamahela, Tarafa ya Kilimatinde wilaya ya Manyoni.

Akielezea mazingira ya ajali hiyo, Kamanda Magiligimba alisema kwamba, Mbunge huyo aliyekuwa akirejea jimboni kwake Manyoni akitokea mjini Dodoma kwa gari aina ya Toyota Prado alimgonga mwanafunzi huyo aliyekuwa kuvuka kutoka upande wa kulia kwenda kushoto wa barabara.

Kamanda huyo alisema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva Mtuka, kushindwa kuchukua tahadhari kwa watumiaji wengine wa barabara.

“Mtuhumiwa mbunge Mtuka anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano na baada ya mahojiano, atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayomkabili. Mwili wa marehemu (mwanafunzi) umehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Manyoni kwa uchunguzi wa daktari na baada ya hapo,utakabidhiwa kwa ndugu kwa hatua za mazishi,” alisema Kamanda wa Polisi.

Comments

error: Content is protected !!