Mwenyekiti wa Usajili Simba, Zacharia Hanspope akamatwa usiku uwanja wa ndege

448
0
Share:
Share this
  • 711
    Shares

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Klabu ya Simba, Zacharia Hanspope amekamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) muda mfupi baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Hanspope aliwasili nchini saa 7 usiku wa kuamkia jana (Oktoba 15) na ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ) akitokea nchini Marekani alikokuwa akipatiwa matibabu.

Mapema mwezi Aprili mwaka huu, TAKUKURU ilitangaza dau la shilingi milioni 10 kwa yeyote atakayefanikisha kupatikana kwa mfanyabiashara huyo na mwenzake Frank Lauwo ambao waliongezwa kwenye kesi ya utakatishaji fedha na kughushi inayowakabili Rais wa Simba, Evans Aveva na Makamu Geofrey Nyange (Kaburu).

Taarifa kutoka ndani ya TAKUKURU zinaeleza kuwa mtuhumiwa huyo aliyekamatwa kwa amri ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu atafikishwa mahakamani leo.

Mahakama ilitoa amri watuhumiwa hao wakamatwe baada ya Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Leonard Swai kudai amewatafuta washtakiwa hao tangu Machi mwaka huu bila mafanikio na kuomba hati ya kuwakamata washtakiwa hao ambao hawakuwepo mahakamani.

Tangu walipokamatwa mwaka jana, Aveva na Kaburu ambao wanakabiliwa na mashtaka 10 tofauti bado wapo rumande huku kesi yao ikiendelea mahakamani.

Comments

error: Content is protected !!