Ripoti ya Mkaguzi Mkuu: Mambo yaliyochangia hasara ya shilingi bilioni 1.5 NIDA

289
0
Share:
Share this
CMTL Group

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), imepata hasara ya TZS 1,469,592,050.98, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hasabu za Serkali (CAG) imethibitisha hilo.

Katika ripoti hiyo, CAG Prof. Juma Assad ameonesha kuwa, hasara ya NIDA imetokana na mambo makubwa matatu ambayo ni, upangishaji wa majengo ya Ofisi za NIDA; malipo yaliyofanyika kwa kutumia viwango tofauti vya kubadilishia fedha za kigeni; na malipo yanayohusiana na ushauri elekezi wa kisheria.

Kwanza, ukaguzi umebani kuwa, kulikuwa na udanganyifu wa mita za mraba katika upangishaji wa ofisi katika jengo la BMTL uliosababisha mamlaka hiyo kupata hasara ya Shilingi 402,210,885.02.

Mamlaka iliingia Mkataba na kampuni ya BMTL mwezi Januari 2012 kwa ajili ya kupanga jengo la BMTL lililopo Victoria, Kijitonyama – Dar es Salaam kwa matumizi ya ofisi.

Uhakiki wa mkataba na vipimo katika jengo husika (ghorofa ya pili na ya tatu) ulibaini kuwa eneo la mita za mraba (m2 ) 2,201 zilizoainishwa katika mkataba halikuwa sahihi. Eneo halisi ni mita za mraba (m2 ) 1,946.9. Hali hiyo imesababisha mamlaka kutozwa zaidi kwa mita za mraba (m2 ) 254.1 isivyostahili, hivyo kupata hasara ya jumla ya Shilingi 402,210,885.02.

Ukaguzi maalum ulibaini kuwa menejimenti ya BMTL walikuwa wakifahamu kasoro hizi lakini walileta madai yao na kulipwa na NIDA.

Pili, ukaguzi umebaini kuwa, NIDA ilipata hasara ya Shilingi 167,445,671.96 kwa kutumia viwango vya benki za biashara badala ya viwango vya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kinyume na mkataba.

Ilibainika kuwa, NIDA ilifanya malipo ya jumla ya Shilingi 12,538,099,500 kwa Kampuni ya Gotham International Limited (GIL) kama Mshauri Elekezi wa Mradi wa Vitambulisho vya Taifa yaliyokuwa yakitozwa kwa Dola za Marekani.

Malipo yalifanyika kwa kutumia Shilingi ya Tanzania kwa viwango vya kubadilishia fedha vya Benki za Biashara vya siku husika badala ya viwango vya kubadilishia fedha vinavyoainishwa na Benki Kuu ya Tanzania kinyume na matakwa ya mkataba husika, hivyo kupelekea mamlaka kupata hasara ya jumla ya Shilingi 167,445,671.96.

Tatu, CAG amebaini kuwa, NIDA ilifanya malipo ya ushauri elekezi mara mbili na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 551,500 sawa na Shilingi 899,935,494.

Ukaguzi ulithibitisha kuwa mkataba wenye thamani ya Dola za Kimarekani 9,000,000 wa miaka mitano (5) kati ya NIDA na Gotham International Limited (GIL) ulisainiwa tarehe 14 Januari 2010 kwa ajili ya kazi ya Ushauri Elekezi, ikiwemo Ushauri Elekezi wa Kisheria wa Mradi wa Vitambulisho vya Taifa.

Pia, ilibainika kuwa, NIDA iliingia mkataba mwingine na M-S Law Partners mnamo tarehe 7 Novemba 2011 wenye thamani ya Dola za Kimarekani 551,500 kwa muda wa miezi mitatu na M/s School of Law (ilijulikana kaam Faculty of Law) kwa ajili ya kazi ya Ushauri Elekezi wa Kisheria kazi ambayo kimsingi ilikwishatolewa kwa Gotham International kupitia Mkataba wake na NIDA.

Hatua hiyo ilisababisha mamlaka kufanya malipo mara mbili kwa kazi moja ambayo ilipaswa kufanywa na Gotham International Limited, suala ambalo liliisababishia mamlaka hasara ya jumla ya Dola za Marekani 551,500 sawa na Shilingi za Tanzania 899,935,494.

Ukaguzi huu maalum kwa ujumla umebainisha mapungufu katika upangishaji wa jengo la Ofisi ya NIDA, gharama zaidi katika malipo kutokana na kutumia viwango vya kubadilishia fedha visivyokuwa vya Benki Kuu kinyume na makubaliano. Vilevile mamlaka ililipia huduma za kisheria ambazo hazikutolewa.

Kufuatia hali hiyo, CAG ametoa mapendekezo kuwa, NIDA ihakikishe fedha zote ilizoilipa Kampuni ya BMTL (sasa The Copy Cat Tanzania Ltd) na Gotham International Limited zinarejeshwa pia inawachukulia wahusika hao hatua stahiki.

 

Comments

error: Content is protected !!