Serikali yaagiza Lazaro Nyalandu achunguzwe

644
0
Share:
Share this
  • 1K
    Shares

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla ameagiza Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) kuanza mara moja kumchunguza aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, Lazaro Nyalandu kufuatia tuhuma mbalimbali zinazomkabili.

“Mimi nitaagiza hapa TAKUKURU pamoja n Jeshi la Polisi wasikilize haya ninayoyasema wayachukue wakafanye uchunguzi ili waweze kumchukulia hatua ndugu Nyalandu,” amesema Waziri Kigwangalla.

Waziri Kigwangalla ameyasema hayo Bungeni Dodoma leo, Novemba 13, ambapo alitaja tuhuma zinazomsukuma kuchukua hatua hiyo.

Baadhi ya tuhuma zilizotajwa dhidi ya Nyalandu ni pamoja na  kutosaini sheria ya tozo kwa hoteli za kitalii alipokuwa waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, ambayo iliikosesha serikali mapato ya Sh32 bilioni kwa miaka ya 2014 na 2015 pamoja na kutumia helkopta ya mwekezaji anayetuhumiwa kwa ujangili kipindi cha kampeni 2015.

“Wakati ndugu Nyalandu akifanya yote hayo, mezani kwake kama Waziri wa Maliasili na Utalii, kulikuwa kuna ‘consection fees’ (tozo) iliyopendekezwa na TANAPA na gazeti likatengenezwa likisubiri signature (saini) ya Waziri ili serikali ianze kuchaji consection fees (tozo) kwenye mahoteli ya kitalii,”

“na hilo lingeongeza mapato na kwa mwaka huo wa 2014 tungeweza kukusanya bilioni 16 lakini Waziri yule hakusaini hiyo GN mpaka anaondoka madarakani. Maana yake Ndugu Nyalandu aliikosesha serikali mapato ya Takriban bilioni 32,” alisema Waziri Kigwangalla.

Lazaro nyalandu, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii katika serikali ya awamu ya nne chini ya uongozi wa Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, hivi karibuni alitangaza kujivua uanachama na nafasi zote za uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na ubunge wa Jimbo la Singida Kaskazini na kuomba kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleao (CHADEMA).

Comments

error: Content is protected !!