Serikali yamzuia Yusuf Manji kurejea Yanga kwa ‘mlango wa nyuma’

431
0
Share:
Share this
  • 698
    Shares

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, amemtaka Mfanyabishara Yusuf Manji kuchukua fomu na kugombea nafasi ya kuwa Mwenyekiti wa Yanga kama bado anamapenzi na klabu hiyo.

Waziri Mwakyembe pia amewaonya wale wote wanaopinga uchaguzi wa klabu hiyo waache mara moja. Hayo yamekuja ikiwa ni siku chache tu baada ya Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini Yanga, Kapteni Mstaafu, George Mkuchika, kutangaza kuwa Manji atarejea katika nafasi hiyo mwakani 2019 pindi afya yake itakapoimarika.

Mei 20, 2017 Manji aliandika barua ya kujiuzulu nafasi ya uenyekiti wa Yanga akiwa nchini Uingereza, ambapo aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga, alichukua nafasi kuwa mwenyekiti na kuiongoza klabu hiyo.

“Tusicheze hii ni Serikali, achukue fomu agombee au wamchukulie, tulipata tabu sana pale Manji alipojiweka pembeni kwani Yanga ilitakiwa kushiriki kwenye mashindano ya kimataifa lakini ilikuwa haina fedha.”

“Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wadau ambao si viongozi walijitutumua kuchangia chochote, lakini hakuna hata senti tano iliyotoka kwa Mwenyekiti huyo wanayemlilia leo, tumechoka kuwabeba, umefika wakati Yanga ichague viongozi wake na tuione ikisimama kwa miguu yake, hilo ndilo lengo la Serikali, tumeichoka kuwa ombaomba.”

“Kama kuna wana Yanga wanaona wataugua bila kuwapo Manji, basi wanaweza kumshawishi achukue fomu agombee lakini si kupitia njia ya mkato, kwanza wachague viongozi ambao wana uchungu na timu hiyo,” alisema Waziri Mwakyembe.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ally Mchungahela, ameshikilia msimamo huo huo na kusema kuwa uchaguzi wa Yanga upo pale pale na wanaotaka kuwa mwenyekiti wachukue fomu.

“Sisi uchaguzi unaendelea kama kawaida, hata nafasi ya Manji pia watu wanachukua fomu kama tulivyoelekezwa na Serikali.

“Kama Manji wanamtaka aendelee kuongoza basi waje wamchukulie fomu au aje achukue fomu, sisi tunafuata taratibu,” alisema.

Kwa upande wake, Rais wa TFF, Wallace Karia, amesisitiza iwe isiwe lazima klabu ya Yanga ifanye uchaguzi, kama walivyoelekezwa na Serikali kupitia Baraza la Michezo Tanzania (BMT).

“Sina la kusema lakini niwaambie neno moja, uchaguzi lazima ufanyike kutokana na agizo la Waziri Mwakyembe, hakuna kitakachozuia watambue wasitambue sisi haituhusu,” alisema Karia.

Comments

error: Content is protected !!