Taarifa ya Clouds baada ya serikali kuzuia Fiesta kufanyika Uwanja wa Leaders

440
0
Share:
Share this
  • 1.2K
    Shares

Clouds Media Group (CMG) imesitisha tukio la kilele cha tamasha la muziki la Fiesta lililokuwa limepangwa kufanyika leo katika Uwanja wa Leaders Club jijini Dar es Salaam.

Uamuzi huo umekuja baada ya serikali kuzuia tamasha hilo kufanyika katika uwanja huo na kuwataka waandaaji kulihamishia katika Uwanja wa Tanganyika Packers uliopo Kawe jijini Dar es Salaam, kwa kile kilichoelezwa kuwa, muziki unaopigwa katika eneo hilo unawaathiri wagonjwa waliopo jirani na eneo hilo.

Katika taarifa ya CMG wameeza kutoa shukrani zao dhati kwa wale wote waliofanikisha tamasha hilo la muziki tangu lilipoanza mkoani Morogoro mwaka huu, na kusema wamefikia uamuzi wa kuahirisha kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao.

“Kwa masikitiko makubwa tunatangaza kusitisha tukio la kilele cha msimu wa Tigo Fiesta 2018 lililopaswa kufanyika leo Novemba 24, 2018 katika Viwanja vya Leaders Kinondoni, Dar es Salaam. Sababu zilizopelekea kusitishwa kwa tukio hili ziko nje ya uwezo wetu,” ilieleza taarifa hiyo.

Kampuni hiyo pamoja na wadau wengi wamewaomba radhi watu wote walioathiriwa  na tukio hilo.

Aidha wameeleza kuwa watarejesha fedha za watu wote waliokuwa wamenunua tiketi, na kwa wale walionunua kawaida, waende kwenye maeneo waliyonunua na watarejeshewa fedha zao.

Comments

error: Content is protected !!