Taifa Stars yaingia makubaliano magumu na Rais Dkt Magufuli

474
0
Share:
Share this
  • 818
    Shares

Unachoweza kusema ni kuwa, timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars imeingia kwenye makubaliano magumu na Rais Dkt John Pombe Magufuli baada ya kutakiwa kushinda mchezo wao unaokuja dhidi ya Lesotho ili kujiweka katika njia salama ya kuweza kufuzu kwa fainali za mataifa ya Afrika zitakazofanyika nchini Cameroon mwaka 2019.

Akizungumza na wachezaji hao Ikulu jijini Dar es Salaam leo, Rais Dkt Magufuli ametoa shilingi milioni 50 ili kusaidia shughuli mbalimbali za timu hiyo wakati ikiwania nafasi ya kushiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 38.

Viongozi wa TFF wakizungumza mbele ya Rais Dkt Magufuli walisema kuwa wanachangamoto ya kifedha ili kuweza kuhakikisha timu hiyo inajiandaa kikamilifu na kushinda mechi zake mbili, dhidi ya Lesotho itakayocheza ugenini na dhidi ya Uganda, itakayocheza nyumbani.

Rais Dkt Magufuli amesema timu hiyo isiposhinda na kufuzu fainali hizo itakuwa imemsikitisha sana na atakwazika kwanini ametoa fedha za walipakodi kwa timu hiyo na imeshindwa kufuzu fainali hizo.

Timu hiyo imeuahidi Rais Dkt Magufuli kuwa itapigana kufa na kupona kuhakikisha kuwa inafuzu fainali hizo, ambapo pia imemshukuru Rais Dkt Magufuli kwa mchango wake wa fedha pamoja na kutenga muda wake kwa ajili ya kukutana nao, na kula nao chakula cha mchana Ikulu.

Tanzania ilishiriki fainali za mataifa Afrika mwaka 1980 zilizofanyika nchini Nigeria. Hii inamaanisha kuwa chini ya utawala wa Rais Mstaafu Mzee Mwinji, Mzee Benjamin Mkapa, na Dkt Jakaya Kikwete, timu hiyo haikuwa kucheza fainali hizo.

Comments

error: Content is protected !!