Takukuru yatangaza zawadi nono kwa atakayefanikisha kukamatwa kwa mtumishi wake

577
0
Share:
Share this

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa TAKUKURU, imetangaza dau nono la shilingi milioni 10, kwa yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa Godfrey Gugai, aliyekuwa mfanyakazi wa TAKUKURU.

“Wananchi popote pale watakapompata au watakapomuona huyu bwana, watoe taarifa katika chombo hichi cha kuzia na kupambana na rushwa na taasisi hii itamzawadia mtu yeyote ambaye atafanikisha kupatikana kwa huyu mtu zawadi ya milioni 10 taslimu,” amesema Mbungo.

Naibu Mkurugenzi wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali, John Mbungo, ameyasema hayo leo alipokuwa anazungumza na waaandishi wa habari na kueleza kuwa Godfrey Gugai anatuhumiwa kwa kujipatia mali nyingi kuliko kipato chake jambo ambalo ni kinyume na sheria ya Utumishi wa Umma.

Brigedia Jenerali, john Mbungo ameeleza kuwa kwa nafasi ya uhasibu aliyokuwa nayo Godfrey ni vigumu kujipatia mali nyingi kiasi hicho, na tayari walishaanza kumhoji lakini baadae alitokomea kusikojulikana.

“Awali tulipomhoji alitoa ushirikiano lakini tukiwa tunaendelea alitoweka na kwa taarifa tu amekuwa akitoka kwa magendo nje ya nchi,” amesema Mbungo.

Ameongeza kuwa baada ya kutoweka walienda mahakamani ambapo waliweka zuio la mali zake kutumika ama kuendelezwa mpaka pale watakapompata na kumuhoji ili kujiridhisha uhalali wake.

“Kama atakuja na kutupa ushirikiano ikiwamo kuthibitisha uhalali wale basi tutamwachia mali yake¬†lakini kwa nafasi yake kumiliki mali zote hizi zinatutia walakini,” amesema.

Mali zilizozuiwa ni pamoja na magari matano, nyumba zaidi ya 5 pamoja na viwanja zaidi ya 30 katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

Aidha Brigedia Jenerali, Mbungo amewataka watumishi wote wa Umma kutotumia vibaya madaraka waliyopewa kwani wakibainika sheria itachukua mkondo wake.

Comments

error: Content is protected !!