Uamuzi wa serikali kuhusu mafao ya waliokutwa na vyeti feki

653
0
Share:
Share this
CMTL Group

Serikali imetangaza msimamo wake kwa watumishi waliobainika kuwa na vyeti feki na wasiokuwa na vyeti vya kidato cha nne kwamba hawana madai yoyote serikalini.

Watumishi waliokosa sifa na vyeti feki, waliagizwa kujiondoa kwenye utumishi wa umma mwaka 2016 na Rais John Magufuli alitangaza kufanyika kwa uhakiki na takriban watumishi 10,000 walibainika.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dk. Laurean Ndumbaro, kwenye kikao cha Kazi cha kujadili masuala ya utawala na rasilimali watu kwa mamlaka za serikali za mitaa, wizara na mikoa, Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Sera, Mathias Kabundugulu, alisema uhakiki wa vyeti ulihitimishwa Oktoba, mwaka jana.

Alisema wote waliobainika waliamuriwa kuondoka wenyewe na wamefutwa kwenye orodha ya watumishi wa umma na hawana madai yoyote serikalini na huo ndio msimamo wa serikali.

Hata hivyo alisema pamoja na uhakiki kukamilika kwa muda uliopangwa, wako baadhi ya maofisa utumishi wameendelea kuwafumbia macho watu wasio na vyeti vya kidato cha nne.

“Wiki iliyopita tulipata barua kuna halmashauri ya Kwimba watumishi kwenye taarifa zao wamejaza wamehitimu kidato cha nne lakini wakati wa uhakiki watumishi hao hawakutakiwa kuwasilisha vyeti husika kwa kigezo wana elimu ya darasa la saba,” alisema Kabundugulu.

Alisema watu wa aina hiyo wamefichwa huko kwenye halmashauri kwa makusudi au bahati mbaya lakini wakumbuke kuna watu wamesoma nao, hivyo ni rahisi kupatikana taarifa zao.

“Tuliagiza maofisa utumishi wa halmashauri na wakurugenzi wachukuliwe hatua na hao maafisa tayari hatua zimechukuliwa kwa upande wa Mkurugenzi wa Halmashauri tumeachia mamlaka yake ya uteuzi,” alisema Kabundugulu.

Alisema serikali ililivalia njuga suala la vyeti feki na watumishi hewa na halijaisha na kwamba watakuwa wanafanya ukaguzi wa kushtukiza na kuchukua hatua.

“Uhakiki huu ni endelevu, hatukutarajia kama tungekuta mtu ana vyeti feki juzi huko. Kuna watu wameshindwa kusimamia vyema, ondokeni hapa mkitambua kuwa tunaendelea, mkawafichue wale wote wenye vyeti feki,” alisema.

Pia aliwataka kuhakikisha wanawaondoa watumishi waliokosa sifa kwenye orodha ya mishahara na kwamba watu hao hawana madai yoyote serikali.

Februari 9, mwaka huu, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu serikali kulipa malimbikizo ya watumishi, alisema serikali imeokoa Sh. Bilioni 84.22 sawa na asilimia 66 ya malimbikizo ya awamu baada ya kuwaondoa kwenye mfumo wa malipo ya mishahara watumishi hewa, wenye vyeti feki na wasio na sifa.

Comments

error: Content is protected !!