Ushauri wa serikali kwa wanafunzi waliokosa mikopo

1101
0
Share:
Share this
  • 1.4K
    Shares

Serikali kupitia Wizara ya elimu, imewataka wanafunzi wote wa elimu ya juu ambao hawajapata mikopo wachangamkie fursa ya kukata rufaa iliyotolewa na bodi ya mikopo kuanzaia jana, Jumatatu, Novemba 13, mpaka jumapili, Novemba 19, mwaka huu.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako aliyasema hayo bungeni jana (Novemba 13) ambapo aliiagiza Bodi ya Mikopo kupitia majina yote ya wanafunzi waliopata na ambao hawajapata mikopo ili kuhakikisha kama mikopo imewafikia walengwa.

“Tayari nimeiagiza Bodi ya wakurugenzi wa Bodi ya mikopo kupitia jina moja baada ya jingine ili kujiridhisha kwamba je, wale waliopangiwa mikopo ndio wenye uhitaji kuliko wale ambao hawjapangiwa lakini pia kupitia majina yote ya wanafunzi ambao hawajapata mikopo ili kujiridhisha kama kweli hawana vigezo kwa mujibu wa vigezo ambavyo vimewekwa,” alisema Waziri Ndalichako.

Aliongeza kuwa sera ya Serikali ni kutoa mikopo kwa wanafunzi wenye uhitaji na siyo kwa wanafunzi wote kama wengi wanavyodhani kwani bado haijafikia kiwango cha kutoa mikopo kwa wanafunzi wote wa elimu ya juu.

“Serikali inatekeleza sera ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wenye uhitaji tu…. Sera yetu ya elimu ya juu ni sera ya uchangiaji, hatujafikia mahali ambapo serikali inatoa mikopo kwa wanafunzi wote na ndio maana hata sheria ya bodi ya mikopo imeaninisha wazi kuwa mikopo itatolewa kwa wanafunzi wenye uhitaji. Kwa hiyo kazi ya Wizara yangu ni kusimamia na kuhakikisha kwamba wale wanaopangiwa mikopo ni wenye uhitaji tu na si vinginevyo,” alisema Prof. Ndalichako.

Aidha siku ya Jumatatu, Novemba 13, mwaka huu, bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ilitoa taarifa kuhusu mambo wanayotakiwa kuyafanya wanafunzi wote wanaotaka kukata rufaa kama inavyosomeka hapa chini.

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inapenda kuwataarifu waombaji wote wa mikopo kuwa dirisha la rufaa litafunguliwa kwa siku 7 kuanzia Jumatatu, Novemba 13 hadi Jumapili, Novemba 19, 2017. Waombaji wote wa rufaa wanapaswa kufuata hatua zifuatazo: –

(i)    Mwombaji anapaswa kukamilisha taarfa zote katika fomu ya maombi mtandaoni, na kuichapisha, kisha kuambatanisha vielelzo vyote vinavyohitajika au barua inayoeleza sababu za yeye kukata rufaa. Fomu za rufaa mtandaoni zinapatikana kupitia http://olas.heslb.go.tz 

(ii)    Baada ya kukamilisha  kujaza fomu ya maombi ya rufaa, mwombaji anapaswa kuipakua kisha kuambatanisha na nakala ya vyeti vilivyothibitishwa (certified documents)  na mamlaka husika kisha kuzifikisha kwa Afisa wa Taasisi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.

(iii)    Malalamiko yote yanapaswa kupitishwa na Maafisa wa Bodi ya Mikopo ambao watakusanya fomu zote za kukata rufaa kutoka katika Taasisi zao na kuzifikisha Bodi ya Mikopo Novemba 21, 2017.  Bodi haitopokea malalamiko yoyote ambayo yatakusanywa moja kwa moja na mwanafuzi.

(iv)    Bodi itapokea na kuchunguza malalamiko yote na pale itakapojiridhisha itarekebisha mkopo au kutoa mkopo mpya kwa waombaji ambao maombi yao ya mikopo yalipigwa awali na Bodi.

Ni nani anayeweza kukata rufaa dhidi ya ugawaji wa Mikopo? 

Mbali na vigezo vya jumla vya ustahiki vilivyotolewa katika Miongozo na Vigezo vya utoaji wa Mikopo na Misaada kwa mwaka wa kitaaluma 2017/2018, mwombaji anahitaji kutekeleza yafuatayo:
    Lazima awe mwanafunzi aliyekubaliwa kuanza au kendelea na diploma/shahada katika Taasisi ya Elimu ya Juu ya Tanzania inayokubaliwa.
    Anapaswa kuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza aliyekuwa ameomba mkopo  au mwanafunzi anayeendelea na masomo aliyeomba mkopo kwa mara ya kwanza kwa mwaka 2017/2018 au mwanafuzi anayenufaika na mkopo.
    Wanafunzi ambao hawakuomba mkopo kwa mwaka 2017/2018 hawatakiwi kukata rufaa.

IMETOLEWA NA:
MKURUGENZI MTENDAJI
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
Novemba 12, 2017

Comments

error: Content is protected !!