Wanaotuma SMS za utapeli wafikishwa mahakamani

1039
0
Share:
Share this
  • 1.7K
    Shares

Watu 13 wamefikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo Agosti 7, 2018  wakikabiliwa na makosa mbalimbali pamoja na uhujumu uchumi ikiwemo utakatishaji fedha wa shilingi milioni 154.

Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga akisoma mashtaka matano yanayowakabili watuhumiwa hao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kelvin Mhina ambapo amedai kuwa washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 5 ambayo wameyatenda katika mikoa mbalimbali.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni, Boniface Maombe, David Luvanda, Moshi Sungura, Amos Bosco, Lule Kadenge, Jofrey Kapangamwaka na William Nturo.

Washtakiwa wengine ni pamoja na Regius Mauka, Collins Basham, Francis Kapalata, Kasonde Kapela, Enock Mwandaji na Pascal Kiatu.

Akisoma shtaka la kwanza, wakili wa serikali alisema watuhumiwa wote wanakabiliwa na shtaka la kula njama kutenda kosa ambapo wanadaiwa wamelitenda kati ya Machi 2018 na Juni 2018 katika jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Rukwa na katika maeneo mengine ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Shtaka la pili linalowakabili ni la kusambaza taarifa za uongo kupitia mfumo wa kompyuta ambapo wanadaiwa wamelitenda Machi na Juni 2018 wakiwa Dar es Salaam na Rukwa ambapo walichapisha taarifa fupi za jumbe (messages) ili kujipatia vitu kwa njia zisizo halali.

Akisoma shtaka la tatu, Wakili Katuga amesema, washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la kusambaza jumbe (messages) kwa njia ya kielektroniki kati ya Machi na Juni 2018 kwa nia ya kudanganya na kushawishi katika mikoa ya Dar es Salaam na Rukwa kwenda kwa watu mbalimbali ili kuonesha wana mamlaka hayo.

Kosa la nne linalowakabili ni kusambaza jumbe fupi za kielektroniki. Wanatuhumiwa kutenda kosa hilo kati ya Machi na Juni 2018 katika mikoa ya Dar es Salaam na Rukwa.

Kosa la mwisho linalowakabili ni utakatishaji fedha ambapo wanadaiwa wamelitenda kati ya Machi na Juni 2018 katika maeneo ya Dar es Salaam na Rukwa. Kwa pamoja watuhumiwa hao wanahusishwa na ufanyaji wa muamala wa shilingi milioni 154,032,830 ikiwa ni zao la kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Baada ya kusoma mashtaka hayo, Wakili wa Serikali, Kelvin Katuga ameiambi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa, upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Kutokana na kuhusisha shtaka la uhujumu uchumi, Hakimu Mhina amesema kesi hiyo haina dhamana, hivyo watuhumiwa wamepelekwa rumande na kesi hiyo imeahirishwa hadi Augosti 21, 2018.

Comments

error: Content is protected !!