Watumiaji wa mtandao wa Twitter Tanzania walivyochangisha zaidi ya shilingi milioni 30 ndani ya saa 12

821
0
Share:
Share this
  • 72
    Shares

Jana (Julai 25 2018) Watanzania wanaotumia mtandao wa Twitter (Tanzanians on Twitter/TOT) waliweka rekodi ya hamasa ya kuchangia jamii kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii chini Tanzania, baada ya kufanikiwa kuchanga zaidi ya shilingi milioni 30 kwa ajili ya matibabu ya Anorld Anthony.

Anorld ni mwanafunzi wa mwaka wa tano katika Chuo cha Tiba cha Hospitali ya Rufaa ya KCMC Moshi, Kilimanjaro (KCMUCo) ambaye ni yatima na amekuwa akisumbuliwa na tatizo la figo kwa muda mrefu ambapo figo zake hazifanyi kazi hivyo anatakiwa kubadili figo hizo.

 

Taarifa kutoka chuoni hapo zinaeleza kuwa, mwaka jana alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu, lakini baadaye alipofanya vipimo aligundulika kuwa figo zake zote hazifanyi kazi ndipo wakaanza kuzisafisha lakini tiba halisi inapaswa kuwa ni kuzibadili.

Watu mbalimbali walioguswa na jambo hilo wameweza kutoa kile walichonacho ili kufanikisha matibabu yake, ikiaminika kuwa, kwa kumsaidia daktari huyo mmoja, inakuwa ni njia ya kuwasaidia watu wengi zaidi, kwani kupitia kwa huduma ya daktari huyo, watu wengi wataweza kutibiwa magonjwa yao na kuokoa maisha.

Kupitia mtandao wa Twitter, Mbunge wa Bumbuli ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, January Makamba aliweza kuhimiza watu mbalimbali na kuchangisha jumla ya shilingi milioni 31.8. Makamba alichukua hatua hiyo baada ya juhudi za awali zilizoanzishwa na wanafunzi wenzake na Anorld na madaktari wengine mtandaoni.

Mapema jana asubuhi, harambee hiyo ikiongozwa na Waziri Makamba ililenga kukusanya shilingi milioni 10, lakini lengo hilo liliongezeka baada ya Dewji Foundation kutoa changamoto na kueleza kuwa, endapo watumiaji wa Twitter Tanzania wataweza kuchangisha shilingi milioni 15 kabla ya jua kuzama, wao kama Dewji Foundation watatoa shilingi milioni 15 zilizobaki ili kufikisha lengo kuu la shilingi milioni 30.  Hadi jua linazama lengo hilo lilifikiwa ambapo Waziri Makamba aliandika kupitia ukurasa wake wa Twitter;

“Jua limezama huku Bumbuli. Na tumepata shilingi milioni 15. Baadaye nitaorodhesha walio-pledge hapa kwa ajili ya uhakiki/ufuatiliaji. Michango itumwe kwenye akaunti au namba za simu zilizowekwa mabangoni. Au tuma kwa mpambe wangu 0759429315. God bless you all.”

Waziri Makamba ametoa orodha ya majina ya watu na taasisi zilizochangia pamoja na kuweka viwango vya fedha vilivyochangwa;

Mfano wa hundi ya shilingi milioni 15 zilizotolewa na Dewji Foundation kutimiza ahadi waliyotoa katika harambee hiyo

Mbali na wachangiaji hao, imeelezwa kuwa mamia ya watu walituma michango ya moja kwa moja kupitia namba za mawasiliano katika bango la kuhamisha matibabu ya kijana huyo ambalo lilitengenezwa na wanafunzi wenzake kiasi cha kufikia muda ambao namba zake za kupokea pesa zilifikia kikomo na kusababisha changamoto ambayo hata hivyo ilitatuliwa. Imeelezwa kuwa hata kabla ya tangazo hilo kusambaa sana tayari wapo wengine ambao walikuwa wameanza kuchangia. Mmoja wapo ni mchekeshji Lucas Mhavile (Joti) ambapo alipoulizwa kuhusu kuchangia alisema huku akiongeza utani kuwa mchango wake tayari alishautoa.

Kufuatia tukio hilo la jana ambalo limeendelea kutoa sura mpya ya matumizi yenye tija ya mitandao ya kijamii nchini Tanzania, Waziri Makamba alisema jambo hilo linatia moyo sana kwani inaonesha wazi kwamba Watanzania bado wana moyo wa kusaidiana.

Matibabu ya kupandikiza figo nchini Tanzania, yanafanyika katika hospitali mbili ambazo ni Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo Jijini Dodoma na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) iliyopo jijini Dar es Salaam.

 

Comments

error: Content is protected !!