Zitto: Nimekuwa kama mwendawazimu

883
0
Share:
Share this
CMTL Group

Mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kuwa amekuwa kama mwendawazimu kufuatia uchungu mkali uliompata ambao umesababishwa na nyumba yake iliyoungua moto mapema juma lililopita.

Zitto Kabwe ameyasema hayo kupitia simulizi aliyoiweka kwenye ukurasa wake wa Facebook alipokuwa akielezea kisa cha nyumba yake hiyo kuungua moto uliosababishwa na hitilafu ya betri za umeme wa jua.

Katika simulizi hiyo, Zitto amesema kuwa nyumba hiyo aliijenga baada ya ile ya baba yake aliyokuwa akiishi naye awali kubomolewa kupisha ujenzi wa barabara ya lami, na hivyo uchungu mkubwa alioupta ni kutokana na nyumba hiyo kuwa na kumbukumbu nyingi ambazo kila mara zikimjia haishi kuumia.

“Mwaka 2008 wakazi wa Mwandiga tuliokuwa tunaishi kando ya barabara ya Kalinzi tuliagizwa kuvunja nyumba kutoka hifadhi ya barabara. Baba alilipwa fidia na tukavunja. Mwenyekiti wa Kijiji cha Kibingo alinipa eneo kwenye ufukwe wa Mto Mungonya. Nikajikusanya na kuweza kujenga nyumba ndogo ya vyumba viwili.”

Zitto amesema kuwa aliendelea kuiendeleza nyumba hiyo kadiri siku zilizvyozidi kwenda ili kuweza kumudu mahitaji yake.

Nyumba hiyo iliungua moto Septemba 15 mwaka huu ikiwa ni siku moja tu tangu Zitto alipotoka Kigoma akiwa njiani kuelekea Nairobi kwa ajili ya kumuona Mbunge Tundu Lissu ambaye amelazwa akipatiwa matibabu.

“Ajali imetokea siku moja tu baada ya Mimi kutoka Kigoma, tarehe 15 Septemba 2017. Hata hivyo, muda wote wa siku 2 nikiwa nje ya Kigoma, sikupata hisia kabisa. Labda ni kwa sababu ya safari yangu ya Kenya ambayo nayo haikuwa ni kwa jambo la kawaida.”

Baada ya kurejea kutoka Kenya, Zitto amesema kuwa alikwenda kwenye nyumba yake hiyo kutazama mabaki baada ya moto kumsababishia hasara kubwa, na ndipo alipopatwa na uchungu kuona kuwa, nyumba yake iliyokuwa imebeba kumbukumbu kubwa, nyumba yake ya kwanza, sehemu tulivu alipokuwa akiishi, hapapo tena kama alivyopajua.

Licha ya kuwa, aliona gofu hili siku hiyo, kesho yake alirudi tena kutazama nyumba hiyo kwani hakuwa ameamini kile alichokiona. Zitto amesema alijiuliza maswali yale yale, na kupata majibu yale yale, akawa anatazama vitu vile vile ambavyo tayari alikwisha kuviona, hali iliyomfanya awe kama mwendawazimu.

“Kuona gofu mbele ya macho yangu kulinirejesha nyuma na kupata hisia kali sana. Nikakumbuka siku zangu za mwanzo kwenye nyumba hii. Usiku ukilala unasikia muungurumo wa maji ya Mto Mungonya na kupata usingizi mwororo. Nikakumbuka asubuhi kwenye sebule nilivyokuwa nakutana na watu kwa masuala mbalimbli ya kazi za Ubunge. Hakika uchungu wa nyumba ya kwanza ni mkali sana.”

“Nimechungulia chumba nilichokuwa nalala zaidi ya mara moja. Nipo kama mwendawazimu tu maana naangalia kitu kile kile nilichokikagua jana. Namwuliza Mlinzi maswali yale yale ya jana na napata majibu yale yale,” ameandika Zitto Kabwe.

Aidha, Zitto Kabwe amesema kuwa kilichotokea ni ajali kama ajali nyingine na kuna haja ya kuichukulia kivingine au kuhusisha na matukio yanayoendelea kwa sasa nchini, badala yake watu wachukue tahadhari mapema.

“Nimeridhika Kabisa kuwa hii ni ajali tu. Hakuna sababu ya kuitazama Kwa muktadha wa matukio yanayoendelea nchini kwetu hivi sasa. Ni ajali na funzo ni kuchukua tahadhari zaidi.”

Unaweza kuisoma simulizi nzima hapa chini;

Comments

error: Content is protected !!