Zoezi la uhakiki wa vyeti vya udereva lasitishwa

1241
0
Share:
Share this
  • 3
    Shares

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, SACP Fortunatus Muslim ametangaza kusitisha zoezi la uhakiki wa vyeti vya madereva lililoanza hivi karibuni hadi hapo itakapotangazwa tena.

Kamanda Muslim aliyasema hayo jana alipokuwa katika ziara yake ya kikazi akikagua utendaji wa watendaji waliopo chini yake ambapo ameeleza kuwa, ametoa muda wa madereva kwenda kusoma kwani ufahamu mzuri wa alama za barabarani utasaidia kupunguza ajali za barabarani.

Akizungumza na baadhi ya madereva mbalimbali kuhusu ajali za barabarani alisema kuwa, ajali nyingi hutokea kutoka na ushindani unaokuwepo kati ya madereva. Alifafanua kuwa, dereva mmoja anapomuona dereva mwingine amekosea, (mfano kupita gari jingine sehemu isiyoruhusiwa) kwavile wanashindana na yeye anafanya kosa lile lile na mwishoe hutokea ajali ambazo hugharimu maisha ya wapendwa wetu.

Zoezi la uhakiki wa vyeti vya madereva lililenga kubaini kama kuna madereva wanaoendesha magari ambao hawakupata mafunzo stahiki jambo linalowafanya kushindwa kufahamu matumizi sahihi ya barabara na hivyo kupelekea ajali.

Hata hivyo, licha ya lengo zuri la zoezi hilo, lilikosolewa na baadhi ya wadau ambao wengi wao walieleza kuwa, kutokana na kutokuwepo wa taasisi moja inayotoa vyeti vya udereva, mtu anaweza kwenda akatengeneza cheti chake mwenyewe, au akahonga katika shule ya udereva akapewa cheti kinachoonesha amehitimu mafunzo, kitu ambacho sio kweli.

Baadhi walishauri kuwa, badala ya Jeshi la Polisi kuweka nguvu nyingi kwenye kukagua vyeti vya madereva, ni vyema nguvu hiyo ikaelekezwa kurekebisha mfumo wa utaoaji wa leseni za udereva. Pia, walishauri kuwa, bila kujali mtu amesoma wapi udereva, wakati wa maombi ya leseni, kuwepo na mtihani maalum kutoka Polisi ambao utawapima waombaji kama kweli wanauelewa juu ya udereva.

Kabla ya Kamanda Muslim kutangaza kusitisha zoezi hilo, tayari baadhi ya madereva walikuwa wamebainika kuwa na leseni bandia ambazo hazikutolewa na mamlaka husika.

Comments

error: Content is protected !!